Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Shilingi milioni 35 kwa ajili ya matibabu ya Edger Mwakabela maarufu Sativa ambaye anapatiwa matibabu katika hospitali ya Aga khan baada ya kupitia masaibu ya kutekwa na kuteswa.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa kupitia chapisho lake la karibuni alilolitoa katika ukurasa wake wa mtandao wa X (Twitter) ambapo amemshukuru Rais Samia kwa kutimiza ahadi kwa kulipia gharama za awali za matibabu ya Sativa.
“Tumepokea nakala ya malipo kiasi cha 35 milion kwenda Agakhan Hosptali. Leo (Julai 02, 2024) jioni Sativa atafanyiwa upasuaji. Hizi ni gharama za awali tuombe kila kitu kiende sawa na gharama zisiwe kubwa huko mbele. Kuna faida kubwa kwa Mhe Rais kuweka mkono wake katika hili.  Hii ni salamu kwa walioko nyuma ya swala hili” Ameandika Olengurumwa.

Aidha ameeleza kuwa na tumaini na ushauri walioutoa kama THRDC wa kuundwa kwa tume huru itakayochunguza tukio lililomtokea Sativa huku akiwashukuru wadau waliosimama mstari wa mbele katika kuhakikisha Sativa anapata huduma bora kama vile Kiongozi Mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ni Martin Masese na Boniface Jacob ambao walihakikisha taarifa za kupotea kwa Sativa zinajulikama ndani ya majukwaa ya kimitandao na nje ya majukwaa.