Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameisisitiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuhakikisha jengo jipya la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji linatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kuzindua jengo hilo Jumatano, tarehe 25 Septemba 2024, Rais Samia amewasihi maafisa wa halmashauri kutumia ofisi hiyo kwa weledi na kwa kutatua kero za wananchi kwa upendo na uwajibikaji.

“Madhumuni ya serikali kujenga nyumba hizi ni kuleta mazingira mazuri kwa maafisa wetu wanaofanya kazi ndani ya halmashauri hii,” amesema Rais Samia.
Ameendelea kwa kusisitiza kuwa majengo hayo ya kisasa yamewekwa miundombinu bora kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi, na kutoa wito kwa watumishi kuwatumikia wananchi kwa weledi ili kuhakikisha huduma zinazoendana na ubora wa jengo hilo zinatolewa.
“Ofisi hizi zitumike kuondoa kero za wananchi. Mkurugenzi Mtendaji na watumishi wote muweze kulitunza jengo hili kama lilivyo leo, kila tukija lionekane hivihivi,” amesisitiza.
Rais Samia pia ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaokuja kutafuta huduma katika ofisi hiyo wanatoka wakiwa wameridhika, tofauti na walivyoingia.

“Tunataka wakiingia wamekasirika kwa shida, wakitoka wafurahi, wapendeze kama linavyopendeza hili jengo,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Joseph Kashushura amemshukuru Rais Samia kwa ujenzi huo huku akisema kuwa ujenzi huo umechukua miaka mitatu na miezi 36 mpaka kukamilika, na kwamba gharama za mradi mzima ni Shilingi bilioni 3.55 ambazo zilipokelewa kutoka serikalini.

Ameeleza kuwa kabla ya kuhamia kwenye jengo hilo watumishi walikuwa wameparaganyika lakini sasa wananchi wanapata huduma pasina shida kwa kuwa wananchi wako mahali pamoja.
Halikadhalika amesema kuwa jengo hilo limevutia uwekezaji kwa kuvutia taasisi mbalimbali kuwekeza karibu na ofisi zake ikiwamo benki ya NMB huku wakiwa na lengo la kujenga kubwa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa siku za usoni.