Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wakulima wa wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro kuendelea kuzalisha mazao kwa wingi ikiwamo mazao ya chakula na biashara.
Rais Samia ameyasema hayo mbele ya wananchi baada ya kuzindua Hospitali ya Wilaya ya Gairo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro siku ya Ijumaa Agosti 02, 2024 ambapo amesema hivi sasa mazao yote ni ya biashara hivyo wakulima hawana budi kuendelea kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwani masoko ya mazao yapo.
“Nitaongea na Waziri wa kilimo ili kusudi kile kilichofanyika katika mikoa ya kusini ya kupandisha bei ya mazao kifanyike na huku, tuendelee kuzalisha mazao tulime mbaazi, kunde, choroko, mahindi na mazao mengine, zalisheni soko lipo”, amesema Rais Samia.
Aidha amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu ili kusudi viongozi wapate muda wa kutosha kufikiri namna ya kuleta maendeleo.
Sambamba na hayo Rais Samia amewahakikishia wananchi wa Gairo kuwa changamoto zote walizoziwasilisha kwa mawaziri tayari zinafanyiwa kazi likiwamo suala la umeme ambapo kituo kidogo kilichojengwa Kongwa kitasambaza umeme mpaka Gairo na kwa upande wa maji tayari serikali imetoa bilioni 34 kuhakikisha Gairo inapata maji.
“Mbunge amesema, waziri wa TAMISEMI amesema lakini suala la maji hawakulizungumza, sasa ninaambiwa kwamba ndani ya jimbo hilo serikali imeleta bilioni 34, mikataba imeshasainiwa na kazi imeanza ya kuhakikisha gairo inapata maji” Ameeleza Rais Samia.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amesema kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu ya serikali ya awamu ya sita kumejengwa zahanati 32 mpya Gairo na hospitali ya wilaya ambayo mpaka sasa imehudumia Wanagairo 12335.
“Katika kipindi kifupi Gairo haikuwa na hospitali ya wilaya, Gairo ni Wilaya na Halmashauri ya Kimkakati, lakini walikuwa wakitumia kituo kimoja cha afya, ninaomba nikupe taarifa Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), kwa kipindi kifupi umetoa zaidi ya Shilingi bilioni 9, imejengwa hospitali ya wilaya ambayo imekamilika” Ameeleza Mchengerwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Gairo Ahmed Shabiby amesema kuwa Rais Samia ametekeleza miradi mbalimbali aliyoiahidi ndani ya jimbo hilo ikiwamo mahakama ambayo ina mwaka mmoja tangu ianze kufanya kazi, mfereji wa kuzuia maji uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 3 pamoja na kujengwa kwa magereza.
Aidha ameeleza kuhusu ujenzi wa barabara inayounganisha tarafa ya Nongwe, Gairo, Kilosa na maeneo mengine ambapo amebainisha kuwa tayari mkandarasi mtaalamu yupo kazini na hiyo ni juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Wilaya ya Gairo ni wilaya ndogo lakini hi wilaya ina tarafa mbili, isipokuwa miundombinu yake ni mimbovu kuliko mkoa mzima wa Morogoro, tarafa ya Nongwe ni tarafa iliyopo Milimani na hata ukiona ule mito inayoenda Kilosa ambao huleta mafuriko Mvumi na kwingineko yote inatoka Nongwe, tayari tuna mtaalamu mshauri wa kutoa lami Gairo kilomita 55 mpaka Nongwe hadi Kilosa” Ameeleza Shabiby.
Akitoa salamu za mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo Adam Malima amesema kwamba wilaya ya Gairo inasifika kwa mapinduzi ya kilimo hivyo wilaya hiyo inatarajia kuchangia pakubwa kwenye pato la taifa kutokana na kilimo.
Aidha amesema Wilaya ya Gairo imeshuhudia uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya na maeneo mengine hali ambayo imesababisha ukuaji wa hali za wananchi wake kiuchumi na kijamii.