Latest Posts

RAIS SAMIA: DINI ZISIWE CHOMBO CHA UCHOCHEZI, SERIKALI ITAHAKIKISHA AMANI INALINDWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa dini nchini kuchukua jukumu la kulinda amani na utulivu wa taifa, huku akisisitiza kuwa serikali haitamvumilia yeyote atakayetumia uhuru wa kuabudu kuchochea chuki na uhasama.

Akizungumza kwenye Baraza Kuu la Eid 2025 jijini Dar es Salaam, Rais Samia ameahidi kuwa serikali itaendelea kulinda na kusimamia misingi ya Katiba inayohakikisha uhuru wa raia kuabudu na kuhubiri imani zao, lakini akatahadharisha kuwa haki hiyo isiwe kichaka cha uvunjifu wa amani.

“Tumeapa kulinda haki na utu wa kila Mtanzania, hivyo hatutasita kufanya wajibu wetu bila woga. Waswahili husema, mchelea mwana kulia hulia yeye,” amesema Rais Samia.

Rais Samia, ambaye tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha kuwa mgombea wa urais kwa uchaguzi wa Oktoba 2025, amesisitiza kuwa dini zisiingizwe katika siasa.

“Kamwe, viongozi wetu wa dini wasidandie ajenda au vishawishi vya kisiasa na kuvuruga nchi yetu. Badala yake, majukwaa ya ibada yatumike kwa ibada, yasitumike na wanasiasa kufanyia propaganda zao,” amesema.

Pia, ameonya kuwa wataendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wachochezi wa vurugu na wavunjifu wa sheria, huku akiwataka viongozi wa dini kuwadhibiti waumini wao wasijihusishe na uchochezi.

“Matarajio yetu ni kwamba majukwaa haya yatafanya kazi ya kutuliza hali na kuleta amani pale wanasiasa watakapotibua utulivu ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa hotuba yake, Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa dini katika malezi ya kimaadili na itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kujenga taifa lenye mshikamano na maelewano.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!