Latest Posts

RAIS SAMIA KUGHARAMIA MATIBABU YA SATIVA ALIYETEKWA NA KUTESWA

Kiongozi Mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kwamba amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya tukio la Edger Mwakabela maarufu kama Sativa kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa vibaya kwa risasi na watu ambao wanatajwa kutokujulikana, na kumwambia kwamba tukio mithili ya lililofanyika kwa Sativa linachafua R-4 zake.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na ACT Wazalendo Julai 02, 2024, Zitto Kabwe alimtembelea Sativa aliyepo katika Hospitali ya Aga Khan akipatiwa matibabu na kuzungumza naye, na ndipo jitihada za kumtafuta Rais zikafanyika ambapo amemueleza Rais katika viatu vyake kama Amiri Jeshi Mkuu kuwa anao wajibu wa kulinda usalama wa raia.

“Nimemnasihi Ndugu Rais juu ya umuhimu wa yeye binafsi kuagiza ufanyike uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya tukio hili pamoja na mengine ya namna hii. Kama Taifa, tunahitaji kushirikiana pamoja kukomesha mambo ya watu kutekwa, kuuawa, kupigwa na kutupwa misituni, yeye Rais anapaswa kuwa wa kwanza kwenye hili” Ameeleza Zitto katika taarifa hiyo.

Kulingana na Zitto Kabwe, Rais Samia ameahidi kufanyia kazi ushauri wake na kwamba Rais binafsi ameeleza kuwa atabeba gharama zote za matibabu ya Sativa kuanzia sasa mpaka atakapopona kabisa pamoja na kuhakikisha unafanyika uchunguzi wa jambo hilo.

“Ninamshukuru ndugu Rais kwa mwanzo huu. Kila safari ndefu, inaanza na hatua ya kwanza. Ninaamini sasa tutaanza safari ya kwenda kule tunakotaka ambako tabia za kutekana na kutesana zitakomeshwa” Ameeleza Zitto.

Aidha amewashukuru Watanzania wote waliomchangia na wanaondelea kuchanga akisema kuwa hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa kwani aliyoyapitia Sativa yanaumiza na kusikitisha sana.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!