Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari mpya ya Mbambabay katika Ziwa Nyasa, hatua inayotarajiwa kuleta faraja na fursa nyingi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, mkoani Ruvuma, Jumatano, tarehe 25 Septemba 2024, Rais Samia ameeleza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya kuboresha usafiri na biashara katika eneo hilo.
“Faraja yangu ni kwamba miaka kadhaa baadaye bandari hii leo imewekwa jiwe la msingi, na ile ndoto yetu na azma yetu inakwenda kutimia,” amesema Rais, akibainisha kuwa bandari hiyo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani ya Malawi, na biashara itakua zaidi katika ukanda huo.
Rais Samia ameeleza matumaini yake kuwa bandari hiyo mpya itaongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Nyasa na kuongeza kuwa, ni muhimu kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vilivyokubalika.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zinawajibika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mujibu wa mikataba.
Aidha Rais Samia ameeleza kuwa huduma za usafiri na usafirishaji Ziwa Nyasa zinapaswa kuimarishwa pia, akisisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu bora ya kupokea meli za mizigo upande wa pili, katika bandari ya Nkhata Bay nchini Malawi, ili biashara kati ya nchi hizo mbili iweze kufanikiwa.
Rais Samia ametaja kuwa diplomasia ya kiuchumi na biashara huru ndani ya Afrika inahusisha kushirikiana na nchi jirani ili miundombinu iwe bora na ifanikishe biashara. Ameziagiza wizara husika na kamati za ushirikiano kuhakikisha Malawi inaweka miundombinu inayofaa kupokea mizigo kutoka Tanzania.
“Nimemuona Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje yupo hapa, kwa hiyo kupitia kamati zetu za ushirikiano watakwenda kuzungumza na wenzetu kule waweke miundombinu itakayofaa kupokea mizigo itakayotoka Tanzania,” alisisitiza Rais Samia, akionesha matumaini ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Malawi kupitia bandari hiyo mpya.