Latest Posts

RAIS SAMIA: USHIRIKIANO NA AVIV TANZANIA KUBORESHA UZALISHAJI WA KAHAWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa serikali imeongeza uwekezaji mkubwa katika zao la kahawa kwa kuhakikisha kipaumbele kimewekwa kwenye sekta ya kilimo, hususan kupitia ongezeko la bajeti na uimarishaji wa huduma za ugani.

Akizungumza Jumanne, Septemba 24, 2024, wakati wa ziara yake kwenye shamba la kahawa la Aviv Tanzania Limited, mkoani Ruvuma, Rais Samia amebainisha juhudi za serikali katika kukuza uzalishaji wa kahawa na mazao mengine.

“Serikali imetoa kipaumbele kikubwa sana kwenye kilimo na imefanya hivyo kwa vitendo. Kwanza kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo, mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti yetu ilikuwa Shilingi bilioni 460 lakini mwaka huu 2024/2025 bajeti yetu ni trilioni 1.250 kwenye sekta ya kilimo peke yake,” amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa ongezeko hilo lina lengo la kukuza mazao ya kilimo na kuuza nje ili kupata fedha za kigeni. Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa sehemu ya fedha hizo zimetumika kuongeza idadi ya maafisa ugani, jambo ambalo limeongeza uzalishaji wa mbegu bora za kahawa.

“Serikali inazalisha miche milioni 20 kwa mwaka na kuigawa bure kwa wakulima ili tuongeze uzalishaji wa zao la kahawa, aina zote za kahawa, arabica na nyinginezo,” ameongeza.

Rais Samia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na miradi mikubwa kama Aviv Tanzania Limited ili mbegu zinazotolewa kwa wakulima ziwe za ubora unaokubalika kimataifa.

“Tunaposema wakulima wawekewe skimu za umwagiliaji maji wazalishe kahawa, haya ndiyo maeneo ya kuyaangalia… kama ni kutoa miche hapa, basi tuwasaidie au kama ni CSR tuzalishe miche mingi iende kwa wakulima,” amesema Rais Samia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!