Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Godfrey Chongolo, amewataka vijana wa bodaboda kujiepusha na kutotumiwa katika uhalifu wa mpakani, hususani uvushaji wa bidhaa za magendo.
Akizungumza na kikundi cha bodaboda cha Itumba wilayani Ileje akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kukagua shughuli za maendeleo, Mhe. Chongolo amewataka waendesha bodaboda kuwa wazalendo na kushirikiana na vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi hasa mipakani.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametumia jukwaa hilo kueleza fursa kwa vijana wa bodaboda kwa kuwapeleka kwenye mafunzo ya udereva vijana 26 wanaoendesha bodaboda bila leseni na kuwalipia gharama za leseni zao ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya kuendelea kufanya kazi barabarani.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi, amesema wilaya yake iko shwari na inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
DC Mgomi, amesema pia kikundi hicho cha bodaboda kimepatiwa mkopo wa pikipiki 10 na pikipiki mbili za matairi matatu (Guta) kupitia mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.