Mkuu wa mkoa wa Kigoma (CGF) Mst. Mhe Thobias Andengenye amezielekeza Taasisi za Umma na binafsi ndani ya mkoa wa Kigoma kutetea watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino kwa kuwapatia haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kuwathamini, malezi, ulinzi, fursa za kiuchumi na kushirkishwa kimaamuzi katika nyanja zote za Maendeleo.
Andengenye ametoa maelekezo hayo Leo Juni 12, 2025 alipofungua Kongamano la watu wenye ualbino lililofanyika katika Ukumbi wa NSSF Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya kukuza uelewa kuhusu ualbino ambapo kitaifa yatafanyika Juni 13, 2025 mkoani hapa.
Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, mkoa wa Kigoma una jumla ya walemavu 362, ambao kati Yao wanaume ni 187 na wanawake 175, ambapo ameishukuru serikali kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa kundi hilo.
“Mkoa unaendelea kusisitiza vyombo vyote vya Serikali, wadau, Halmashauri kuendelea kusimamia na kutoa haki za msingi kwa kundi hili, huku kipaumbele hicho kikiwa katika uoatikanaji huduma za Afya, Elimu, ulinzi, usalama, ajira, kushirikishwa pamoja na mafunzo ya ufundi Stadi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ualbino Taifa (TAS) Ndg. Godson Mollel amesema kwa upande wao watahakikisha wanafikia maeneo yote wanayohisi hakuna uelewa kuhusu wenye hali hiyo ili kutoa Elimu.
Aidha Molel amesisitiza kuwa kundi hilo litashiriki kikamilifu zoezi la Uchaguzi Mkuu na baadhi yao wameshaonesha nia ya kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi huku akiomba Watanzania kuwaamini na kuwapa nafasi hizo.