Uongozi wa vyama vya wafanyakazi Mkoani Kigoma umetakiwa kuzingatia usawa katika kusimamia haki za waajiri na waajiriwa ili kudumisha utendaji kazi wenye msingi wa kuleta matokeo chanya kwa Umma na upatikanaji wa maslahi kwa Watendaji.
Kauli hiyo imetolewa na mKuu wa Mkoa wa Kigoma alipozungumza na maelfu ya wafanyakazi kutoka Taasisi za Umma na Binafsi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kimkoa iliyoadhimishwa katika wilaya ya Kakonko mkoani hapa.
Amesema waajiri na waajiriwa wanapaswa kuendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri kwani mahali popote pa kazi penye mahusiano mema, ujira mzuri na ulio halali lazima panakuwa na mafanikio na ufanisi katika uzalishaji au utoaji wa huduma.
Amesema wafanyakazi hususani katika Sekta za Umma wanapaswa kuongeza juhudi kiutendaji kazi kwani ni mashuhuda wa namna ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyothamini utendaji kazi wao kwa kuendelea kubooresha maslahi yao ikiwa ni pamoja na kupandisha mishahara na madaraja katika ngazi mbalimbali za kiutumishi.
Kupitia hotuba yake, Andengenye amewataka wafanyakazi kujiimarisha katika matumizi ya Teknolojia pamoja na kujiwekea sera za kupambana na umasiki ili kutoa huduma bora na kuzalisha bidhaa zitakazomudu ushindani kimasoko.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanyakazi mkoani Kigoma kushiriki kikamilifu mchakato wa uchaguzi kwa kujiandijisha na kupiga kura sambamba na kuihamasisha jamii kushiriki zoezi hilo kwa hali ya amani na utulivu.