Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amewataka vijana kuwa tayari kulitumikia Taifa katika nyakati zote kama walivyofanya baadhi ya mashujaa wakati nchi ikipambania uhuru kwani kufanya hivyo ndiyo uzalendo wa kweli.
Malima ameyasema hayo Julai 25, 2024 mkoani Morogoro wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa katika ngazi ya mkoa ambapo ameeleza kuwa maadhimisho hayo hufanyika ili kuyaenzi na kuyasisitiza mazuri yaliyofanywa na mashujaa kwa kizazi cha sasa hivyo ni wakati sasa vijana kujitoa ili kuendelea kudumisha amani katika nchi yao.
Nao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro wamesema kuwa uzalendo na moyo wa kujitoa ambao ulioneshwa na mashujaa waliopigania Taifa la Tanzania ni chachu iliyosabisha uwepo wa amani na utulivu na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yaliyobeba ukombozi wa mataifa mengine yaliyopitia changamoto za uvamizi wa wakoloni, huku wakisisitiza kuwa kizazi cha sasa kinapaswa kuelezwa historia ya Nchi ili kufahamu umuhimu wa uzalendo.