Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amepiga marufuku wananchi kuwarekodi madaktari na kusambaza video au sauti mitandaoni badala yake waweze kutumia njia sahihi ya kutoa taarifa kwa uongozi madaktari wanapokosea.
RC Mtaka ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ukalawa wilayani Njombe baada ya kuzindua kituo kipya cha afya kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 300 fedha ambayo ni kutoka serikali kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe pamoja na nguvu za wananchi.

“Wananchi kuweni na lugha nzuri kwa watoa huduma, ujue kwamba nesi anapokuhudumia pengine wewe ni mtu wa ishirini, sitarajii kuona mwananchi ameenda kuzungumza na mtoa huduma amemrekodi na kupeleka mtandaoni”, amesema Mtaka na kuongeza,
“Utaongea na nesi utamrekodi na kupeleka mitandaoni akatukanwa halafu kesho utapata shida na kurudi, mimi niwaombe kama kuna changamoto yoyote nenda kwa viongozi wake waambie lugha hii imenikwaza na mengine tuvumiliane”
Awali kabla ya kupata kituo hicho cha afya, wananchi wa Ukalawa walikuwa wakifuata huduma umbali mrefu ikiwemo kata ya Lupembe ambapo akitoa ushuhuda wa adha walizokuwa wakikutana nazo, diwani wa kata hiyo Javan Ngumbuke amesema kufunguliwa kituo hicho ni mkombozi mkubwa kwao kwani amewahi kuzalisha wanawake watano kwenye gari yake wakati akisafirisha wagonjwa kufuata huduma.