Latest Posts

RC MTWARA- FEDHA ZA MKOPO ZIPO, SHIDA BAADHI YA VIKUNDI HAVINA SIFA

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amewataka viongozi wa serikali kushirikiana na wabunge na madiwani katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuhusu mapitio ya bajeti ya nusu mwaka wa fedha 2024/2025 na makadirio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Sawala amesema kuwa fedha za mikopo zipo, lakini baadhi ya vikundi hukosa fursa hiyo kutokana na kushindwa kutimiza vigezo.

“Fedha za mikopo zinatengwa, lakini changamoto ni baadhi ya vikundi kushindwa kukidhi vigezo. Ni jukumu letu kuhakikisha tunawasaidia kufanikisha hili,” amesema Sawala.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Mtwara, Abdillah Mfinanga, mkoa huo umekisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 290.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo bilioni 2.9 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10. Kati ya fedha hizo wanawake watapata shilingi bilioni 1.2, vijana – shilingi bilioni 1.2 na watu wenye ulemavu – shilingi milioni 592.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara, Agnes Okololo, amepongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua tena dirisha la mikopo hiyo, akisema kuwa hatua hiyo inasaidia kuchochea maendeleo kwa wanufaika.

“Sasa mfumo wa uombaji ni wa kidijitali, hivyo elimu zaidi inahitajika ili kuhakikisha watu wengi zaidi wanapata fursa hii,” amesema Okololo.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Mtwara unatarajia kupokea ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 62.3, huku fedha za ndani zikiwa bilioni 29.02 (asilimia 46.54) na fedha kutoka nje bilioni 33.3 (asilimia 53.45).

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara inakadiria kupokea na kutumia shilingi bilioni 4.5, ambapo bilioni 2.3 zinatoka kwenye mapato ya ndani (asilimia 51.11) na bilioni 2.1 zinatoka kwenye fedha za nje (asilimia 48.88).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!