Wakulima wa Mkoa wa Mtwara wanatarajia kunufaika na mbegu bora za mazao mbadala baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kukabidhi tani sita za mbegu za ufuta kwa ajili ya kugawiwa bure kwa wakulima.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya mbegu hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza wigo wa uzalishaji wa mazao mengine kama ufuta, mbaazi na choroko, ambayo yatawasaidia wakulima kupata vyanzo zaidi vya kipato badala ya kutegemea korosho pekee.

Amesisitiza pia umuhimu wa wakulima kuandaa mashamba mapema kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaoonesha mvua kuanza mwezi Desemba, ili kuhakikisha mazao yanastawi kwa ubora unaotakiwa kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

RC Sawala ametoa wito kwa wakulima kuendelea kuuza mazao yao kupitia mifumo rasmi ya minada ya kidijitali ambayo imeendelea kuongeza uwazi na kipato kwa mkulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa COPRA Irene Mlola, amesema mamlaka hiyo imejikita kuwaunga mkono wakulima moja kwa moja shambani kwa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani ili kuhakikisha usimamizi wa kitaalamu na uzalishaji wa mazao yenye viwango vinavyokubalika kimataifa.

Mbali na ufuta, COPRA inatarajia pia kutoa tani tatu za mbegu za mbaazi na tani tatu za choroko kwa ajili ya wakulima wa mkoa huo.