






Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Ijangala wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 360 umeanza kuchangia uzalishaji wa umeme katika gridi ya taifa, hatua ambayo imeimarisha upatikanaji na ubora wa nishati katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Mradi huo uliopo katika Kijiji cha Masisiwe, Kata ya Ukwama, leo Jumanne Machi 10, 2026 umetembelewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tanzania Editors Forum – TEF) katika ziara maalum ya kujionea maendeleo ya miradi ya nishati vijijini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yessaya, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya uzalishaji umeme inayoungwa mkono na serikali ili kuongeza uzalishaji wa nishati nchini.
Amesema serikali kupitia REA imekuwa ikitoa ruzuku kwa waendelezaji wa miradi ya nishati kuanzia hatua za awali za maandalizi, ikiwemo kugharamia tafiti za awali za uwekezaji kama upembuzi yakinifu, tathmini ya athari za mazingira na maandalizi ya mpango wa biashara.
“Serikali kupitia REA inasaidia taasisi za serikali na sekta binafsi kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme vijijini ili kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa na kuimarisha ubora na uimara wa nishati,” alisema Yessaya.
Kwa mujibu wa Yessaya, serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 1.63 kusaidia ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.
Aidha, kupitia Mpango wa Upanuzi wa Umeme Vijijini Tanzania (Rural Electrification Expansion Programme – TREEP), mradi huo ulipata mkopo nafuu wa shilingi milioni 922 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za utekelezaji wake.
Akifafanua zaidi, amesema kuwa baadhi ya miundombinu iliyogharamiwa na serikali ni pamoja na transfoma chochezi ya KVA 500 pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 0.6 inayounganisha kituo cha mradi na gridi ya taifa.
Ameendelea kwa kusema kuwa katika Mkoa wa Njombe, REA imefadhili zaidi ya miradi mitano ya uzalishaji umeme wa aina hiyo, ambapo baadhi inaingiza umeme kwenye gridi ya taifa huku mingine ikiwasambazia wananchi moja kwa moja kulingana na leseni walizopata.
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Ijangala, Daud Sanga, amesema mradi huo unasimamiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kusini Kati kupitia Kituo cha Udiakonia cha Tandala kilichopo mkoani Njombe.
Amesema miundombinu yote ya mradi huo imekamilika, ikiwemo jengo la kuzalisha umeme (power house), bwawa la maji, mabomba ya kusafirisha maji na kituo cha kupoza umeme.
“Sasa tangu Machi 2025 tumeanza kuuza umeme kwa kupeleka katika gridi ya taifa,” alisema Sanga.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza kama wazo lililoonekana kuwa gumu, lakini msaada wa REA katika hatua za awali za maandalizi uliwezesha mradi kufanikishwa.
“Sehemu kubwa ya fedha za ujenzi zimetoka REA. Bila msaada huo, pengine tusingefika tulipo sasa,” alisema.
Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo yote ya Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema ushirikiano kati ya REA na TEF unasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu miradi ya nishati inayotekelezwa vijijini huku akisisitiza kuwa, miradi ya wazalishaji wadogo wa umeme ina mchango mkubwa kwa taifa kwa kuongeza umeme katika gridi ya taifa na pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii kupitia ajira na mapato kwa wananchi.
Balile ameishauri REA kuendelea kuunga mkono miradi kama hiyo kwa kuwa inaonyesha jinsi taasisi, makanisa na watu binafsi wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.