Latest Posts

RIPOTI YA TATHIMINI YA SHERIA ZA UCHAGUZI YABAINI WALAKINI RAIS KUCHAGULIWA KWA KURA NYINGI

Uchambuzi uliofanywa na Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) umebaini kuwa vipengele kadhaa vya sheria za uchaguzi zilizopitishwa rasmi mwaka 2024 vinaibua na kuendeleza wasiwasi na mashaka juu ya uthabiti na uadilifu wa mifumo ya chaguzi za Taifa la Tanzania katika kuhakikisha chaguzi huru, za haki na kuaminika.

Hili limedhihirika kupitia ripoti ya JUKATA iliyowasilishwa Jumatatu Juni 10, 2024 kwa wanahabari kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Twaweza East Africa, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wataalam wengine wa kujitegemea ambao walifanya mapitio na uchambuzi wa sheria mpya za uchaguzi nchini.

Sheria zilizofanyiwa uchambuzi ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, Sheria ya Masuala ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Akizungumza katika uwasilishaji wa ripoti hiyo ya tathmini, Mwenyekiti wa Bodi Jukwaa la Katiba Tanzania Dkt. Ananilea Nkya amesema miongoni mwa vipengele vilivyoibua mashaka ni kuendelea na makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi  ambapo amekutaja kutokuonesha mabadiliko ya kuboresha Tume ya Uchaguzi.

Aidha amesema kuwa kukosekana kwa sheria maalumu za kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kama inavyotakiwa na kifungu 10 (c) cha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kunaibua wasiwasi kuhusu uhalali na uwazi wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika kabla ya kutamatika mwaka 2024.

“Kwa sababu uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika Novemba ilitakiwa hadi leo ile sheria inayoelekeza jinsi ambavyo Tume Huru ya Uchaguzi itasimamia uchaguzi iwe tayari ili kuanzia mwaka huu uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi” Amesema Dkt. Nkya.

Mpangilio wa kumchagua Rais wa Tanzania na mamlaka yake navyo vimeangaziwa ambapo Dkt. Nkya amesema kanuni ya kuamua mshindi wa matokeo ya Urais kwa kuangalia mwenye kura nyingi hata kama kamzidi mwenzake kura moja kutangazwa mshindi wa kiti cha Rais inadhoofisha uhalisia wa uwakilishi wa wananchi na pia madaraka makubwa ya Rais ya kuwa mamlaka ya kinidhamu ya kuwaondoa makamishna kwenye Tume kumetajwa kuwa tishio la uhuru wa Tume ya Uchaguzi.

“Kuendelea kuweka marufuku ya kuhojiwa kwa matokeo ya Rais mahakamani kunapoka mamlaka ya Mahakama ya kuwa chombo chenye maamuzi ya mwisho katika kutoa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwanyima fursa ya kuhoji mahakamani wananchi au wagombea ambao hawajaridhika ya uchaguzi wa Raisi” Ameendelea kutaja changamoto hizo Dkt. Nkya.

Waswahili husema kila lililo baya halikosi wema wake, JUKATA imebaini baadhi ya vipengele vya sheria hizo kuwa vizuri katika kukuza uadilifu, haki na imani kwenye chaguzi ikiwa tu vitatekelezwa kikamilifu.

Vipengele hivyo ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, tume kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuondoa ulazima wa kutumia wakurugenzi watendaji kusimamia chaguzi na kuondoa mtindo wa wagombea kupita bila kupingwa kwa kupoka haki ya wapigakura kueleza hisia zao kwa mgombea husika wakati wa uchaguzi.

Licha ya mabadiliko hayo ya sheria za uchaguzi yaliyofanywa na serikali ya Tanzania, JUKATA imeendelea kusisitiza kuhusu upatikanaji wa katiba mpya ikiwa na imani kuwa hakuna mageuzi ya maana ya chaguzi Tanzania yanayoweza kupatikana bila kugusa katiba.

“Matatizo makuu ya uchaguzi mizizi yake inatoka kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Hivyo, tunatoa wito kwa serikali kufanya jitihada za lazima kufanya marekebisho ya kisheria na katiba kukidhi matarajio ya watanzania ya kuwa na chaguzi huru, za haki na kuaminika” Ameeleza Dkt. Nkya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!