Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa chama cha ACT Wazalendo Janeth Rite ameitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya kile alichokiita ‘kucheza upatu maisha ya Watanzania’ akidai wakulima wamekuwa wakinyanyaswa na jeshi la polisi ambalo lina wajibu wa kuwalinda wao na mali zao.
Rite ameyasema hayo siku ya Jumamosi Juali 27, 2024 akiwa katika mkutano wa hadhara wa chama chake uliofanyika Kasulu Mjini, mkoani Kigoma.
“Badala yake kimegeuka kuwa chombo cha kuwanyanyasa raia, wakulima wanachomewa mazao yako kwa kisingizio cha kulima eneo ambalo sio rasmi, kwa unyonyaji huu wa jeshi la polisi limepoteza weledi wa kuitwa jeshi la wananchi badala yake waitwe kikosi cha uporaji na unyanyasaji” Ameeleza Rite.
Aidha Rite amemtaka Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu kuliangalia upya jeshi hilo ambalo ameueleza msaada wake kuwa haba kuliko mahitaji ya Watanzania kutokana na namna linavyoendeshwa.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi kufanya mabadiliko kwa kuchagua viongozi wanaotokana na chama cha ACT Wazalendo lengo likiwa kufanya mabadiliko kuanzia ngazi ya chini na kuondoa utawala wa Chama Cha Mapinduzi unaotajwa kushindwa kuwaletea wananchi yale wanayoyatamani.