Latest Posts

ROSE MHANDO: MSAMA NI BABA KWANGU ACHENI KUNIGOMBANISHA NAYE.

Mwimbaji nguli wa muziki wa Injili Afrika Mashariki na Kati, Rose Mhando amekiri kwamba Mkurugenzi wa Msama Promotions ambaye ni mwandaaji wa matamasha mbalimbali ya muziki wa Injili Alex Msama, ni zaidi ya baba kwake kwani tangu alipoanza kazi zake za uimbaji wa nyimbo za Injili amekuwa akifanya naye kazi kwa wema bila dhuluma na kwamba Msama hajawahi kumdhulumu.

Rose ametoa kauli hiyo baada ya hivi karibuni kuwapo taarifa kwenye mitandao ya kijamii, zikidai msanii huyo aliwahi kudhulumiwa haki zake na Msama.

“Kwangu mimi, Msama ni zaidi ya baba, amenisaidia mambo mengi sana, kuanzia fedha hadi ushauri, amenivumilia hata ninapomkwaza, leo mtu anaweza kuchapisha taarifa na kueleza kwamba eti Msama aliwahi kunidhulumu, hii sio kweli kabisa sjawahi na siwezi kusema kauli hiyo dhidi ya Msama”, amesisitiza Rose.

Mhando amesema yeye na baadhi ya wasanii wenzake wa muziki wa Injili, hawawezi kujivunia mafanikio yao bila kutaja jina la Alex Msama ambaye hivi karibuni alipata tuzo ya Muandaaji Bora wa Muziki wa Injili wa wakati wote

Akizungumzia kuhusu madai hayo, Rose amesema ameshitushwa na kusikitishwa sana na taarifa hizo na kuongeza kuwa hajui zimetokea wapi na watunzi wa uzushi huo wana lengo gani.

Katika maisha yake ya mafanikio ya muziki huo, Malkia huyo wa muziki wa Injili amesema hawezi kusahau jina la Msama akidai kuwa ametumia muda mwingi wa maisha yake na fedha zake kuibua na kukuza na kulea vipaji wa vya muziki wa Injili na kuhakikisha haki zao zinalindwa.

Akitolea mfano, Rose anasema Msama alikuwa anamsaidia kutoa ushauri wakati wa kuandaa muziki, kutoa msaada mkubwa wa fedha kuingia studio na kurekodi na zaidi ya yote alianzisha vita ya kukabiliana na waliokuwa wakiiba na kuuza kanda za CD za kazi za wasanii na kuwafanya wasanii hao kukosa haki zao na kuishi maisha ya shida.

“Yapo mambo madogo ya kibinadamu yaliyowahi kutokea wakati wa kazi, ikiwamo mimi mwenyewe kumkwaza Msama, lakini hiyo haina maana kwamba Msama amewahi kunidhulumu haki zangu”, ameeleza Rose.

Kwa mujibu wa Rose, ataendelea kufanya kazi na Msama wakati wowote atakapohitajika na ataendelea kuwa chini yake kwani anaamini mfanyabiashara huyo ana mapenzi ya dhati ya muziki wa Injili kutoka moyoni na serikali inapaswa kumuangalia kwa jicho tofauti na hata kumpa msaada.

“Mimi na baadhi ya wasanii wenzangu tulifika hatua ya kumuita Msama kuwa ni Askofu wa Muziki wa Injili, yule baba ana mapenzi na muziki wa Injili kutoka moyoni, ni mtumishi wa Mungu aliyeamua kufanya utumishi wake kwa kukuza vipaji vya wasanii wa muziki huo”, ameeleza.

Alimwomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumuangalia Msama na kumlinda pale anaponyanyaswa na baadhi ya watendaji wa serikali, akieleza kuwa kumuua Msama ni kuua ndoto na maisha ya wasanii wa Muziki wa Injili.

Kuhusu hatma yake kwenye muziki huo, Rose amesema muda mrefu amejiweka kando kutokana na changamoto za kiafya, lakini hivi sasa anaandaa albamu mpya ya muziki wake ambayo itazinduliwa wakati wowote mwaka huu.

“Baada ya kutoka hospitali, nilijipa muda wa kupumzika, lakini hivi sasa naandaa Albamu yangu ya kukata na shoka, itazinduliwa wakati wowote mwaka huu na itakapokuwa tayari nitawajulisha washabiki wangu,” Ameeleza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!