Latest Posts

ROYAL TOUR YA RAIS DKT. SAMIA NA ONGEZEKO LA WATALII MISITU YA MAGAMBA, LUSHOTO, TANGA.

Mhifadhi mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Hifadhi ya Magamba wilayani Lushoto mkoani Tanga Christoganus Vyakuta amesema kutokana na filamu ya The Royal Tour aliyotengeneza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wilayani Lushoto kumekuwa na ongezeko la watalii wa nje na wa ndani ambapo hadi kufikia Novemba mwaka 2024, zaidi ya watalii 5000 wamefika kujionea vivutio vya utalii wilayani humo.

Hayo yamesemwa na Mhifadhi mkuu wa TFS Hifadhi ya Magamba Christoganus Vyakuta wakati akizungumzia vivutio vya utalii vilivyomo katika misitu ya Magamba ambako siku ya tarehe 7 mwezi huu kutakuwa na hafla ya matembezi ya watalii katika misitu hiyo.

Amesema katika Lushoto kuna kila kitu kinachohusu utalii ikiwa ni pamoja na kivutio cha hali ya hewa ya ubaridi tofauti na maeneo mengine ya nchi yetu.

”Lushoto kuna hali ya hewa ya baridi ambayo imekuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii wengi hasa kutoka nje ya nchi” amesema Vyakuta.

Amesema kuna siri kubwa sana katika kutembelea utalii wa kimazingira kwani huimarisha afya ya mtalii hasa kutokana na hali ya hewa nzuri ya wilaya hiyo.

Aidha amesema Wajerumani wamekuwa wakifika katika wilayani hiyo kujionea kumbukumbu mbalimbali za wajerumani zilizoanzishwa hapa nchini kipindi cha ukoloni.

Naye Afisa Utalii wilaya ya Lushoto Shadrack Makaya amesema maeneo ya Usambara yamekuwa ni chachu kubwa ya utalii hasa kutokana na vivutio vya kiasili ambapo katika milima ya usambara kumekuwa na njia za kutembea kwa miguu ambazo huvutia watalii.

Amesema pia watu hawajui kuwa hali ya hewa ya baridi nayo ni kivutio kikubwa kwa watalii ikiwa ni pamoja na maporomoko ya maji ambayo yapo sehemu nyingi.

”Kuna watu hawafahamu kuwa kuna utalii baridi ambao umekuwa ukileta watalii wengi sana huku Lushoto tofauti na maeneo mengine, hivyo sasa hivi tumeandaa mikakati kikubwa ya kuweza kuhamasisha watu wengi waje huku, kwani huku muda wote ni baridi kabisa” amesema Makaya.

Amesema Lushoto kuna mapango ya kihistoria ya aina mbalimbali wakiwemo viumbe hai walio katika misitu ya milima ya Usambara na kuvutia wageni.

”Pia Lushoto tuna mawanda ya uono wa juu na chini nyingi sana ambayo ukizunguka pembezoni mwa milima hii utaona uono mbali mbali kama uwanda wa Ilenje, uwanda wa Mambo ambao ukiwa pale juu unaweza kuona Mlima Kilimanjaro vizuri hasa wakati wa asubuhi pamoja na kuona hifadhi ya Mkomazi kwa juu na kuona sehemu ya misitu ya hifadhi ya Tsavo nchini Kenya ukiwa katika uwanda wa juu wa Mambo” amesema Makaya.

”Pia tunaendelea kutunza mila na desturi za kihistoria za makabila ya wazawa kama Wasambaa, Wadigo, Wapare, Wambugu, Wazigua Na Wamasai kwani makabila hayo yalikuwa yakikaa huku ikiwa ni pamoja na kuendelea kutunza historia ya Chifu Kimweri ambaye alikuwa maarufu hivyo tunatunza ili vizazi na vizazi waendelee kujifunza wamfahamu” amesema Makaya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!