Latest Posts

RTO SONGWE: MUWASHAURI VIONGOZI KUHUSU USALAMA BARABARANI

Na Josea Sinkala, Songwe.

Madereva wa magari ya Serikali pamoja na taasisi za umma mkoani Songwe wamekumbushwa kuwa na nidhamu na kuongea barabarani kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Hii ni pamoja na kuwa washauri wa viongozi wanaowaendesha juu ya masuala ya usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika na kulinda usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe (RTO) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Bukombe wakati wa Semina ya utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva hao katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Katika Semina hiyo, SSP Bukombe ameeleza kuwa ni wajibu wa dereva kufuata sheria, alama na michoro ya barabarani ili kuwa salama katika majukumu yake ya kila siku.

Pia amewataka madereva hao kujiendeleza kusoma juu ya taaluma yao kutokana na mabadiliko ya teknolojia ambayo inawataka kujipanga wakati na baada ya maisha ya kazi kwa mstakabali wa maisha yao baada ya kazi.

 

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mbozi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba, amesema katika semina hiyo walijikita zaidi kuwaelimisha madereva hao juu ya madhara ya mwendokasi, kuvipita vyombo vingine sehemu ambazo haziruhusiwi ikiwa ni pamoja na kuchukuwa tahadhari sehemu ambazo ni makazi ya watu ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Vilevile katika Semina hiyo, madereva hao wamekumbushwa sheria mbalimbali za usalama barabarani kutoka kwa afisa wa Polisi Koplo Chika Sanda na Koplo Maganga Kalulumya wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, ambao wamewataka kuwa na kitabu cha sheria hizo ili kujikumbusha kwa lengo la kuendelea kuwa salama kipindi chote cha utendaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na watumiaji wa barabara.

Kwa niaba ya madereva wengine baada ya mafunzo hayo mmoja wa madereva aitwaye Fungafunga Njovu (Dereva kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma) amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa elimu waliyoitoa na kuomba mafunzo hayo yawe endelevu ili kuendelea kuwajengea uelewa madereva juu ya umuhimu wa sheria za usalama barabarani na kuahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa katika masuala ya usalama barabarani kuhakikisha wanakuwa salama wao na watumiaji wengine wa barabara ili kuondokana na ajali zisizo na ulazima.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!