Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wameombwa kuwashirikisha na kuwaelewesha wananchi pindi changamoto zinapojitokeza kwenye miradi yao ili kuwatoa hofu wananchi.
Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ally Usi wakati akizindua ukarabati wa ujenzi wa Mradi wa maji Malamba uliopo Kata ya Mtiniko Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara ambapo zaidi ya wananchi 2,600 watanufaika na mradi huo.
Usi amesema inapotokea changamoto ya aina yoyote ni vizuri kuwafahamisha wananchi ili waweze kuelewa na kuvumilia changamoto husika zitakapojitokeza.
Pia amewataka wananchi kulinda na kuitunza miundombinu hiyo ya maji ili izidi kuwanufaisha na kuwaondolea changamoto ya maji.
“Tuilinde na kuitunza miundombinu hii maji kwasababu naamini wapo wachache wasiopenda maendeleo yanayofanywa katika maeneo yetu,wataenda kutafuta njia yoyote kwenda kuangalia pump za maji zimepita maeneo gani wakatoboe au wakate ili wananchi waliowengi wasipate huduma ya maji.”Amesema Usi
Mhandisi Abdul azizi Hemed amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 100.1 na unatarajia kuhudumia wananchi wa kijiji cha Malamba na Mkulanga ambao wataepukana na changamoto ambayo hapo awali walikuwa wanakabiliana nayo.
Kuluthumu Uwesu mwananchi wa kijiji cha Mkulanga ameishukuru serikali kwa kutoa fedha ambazo zimekarabati miundombinu ya mradi huo na kuweza kuwanufaisha wakazi wa maeneo hayo ambayo ilikuwa inawalazimu kutembea umbali wa kilomita 7 kwaajili ya kufuata maji.
Sambamba na hilo Usi amezindua mradi wa ujenzi wa nyumba tano za makazi ya vijana wa kikundi cha ujasiamali cha Pambamoto zilizojengwa kwa pesa zilizotokana na mkopo wa aslimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri ya mji Nanyamba ambazo gharamab zake ni shilingi milioni 97,817,000 na kuwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuiga mfano kwa kikundi hicho.