Mapema siku ya Jumamosi Julai 27, 2024 zimesambaa taarifa zinazodai kuwa Wakili wa kujitegemea Peter Madeleka anashikiliwa na Jeshi la Polisi kituo cha kati (Central Police) jijini Dar es Salaam ambapo kwa wakati huo haikufahamika mara moja sababu za kushikiliwa kwake
Kufuatia sintofahamu hiyo Jambo TV imewasiliana na Wakili wa kujitegemea Hekima Mwasipu anayefuatilia suala hilo akiwa ndiye Wakili wa Madeleka, ambapo amesimulia kuwa Wakili huyo (Peter Madeleka) alifika Central Police leo kwa ajili ya kumsimamia mteja wake aliyeibiwa fedha Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya kufika kituoni hapo wawili hao (yaani Wakili Madeleka na mteja wake) walielekea kwenye ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, na kukabidhiwa askari kwa ajili ya kuandika maelezo yanayohusu mteja wake kuibiwa fedha kama ilivyoelezwa hapo awali.
Taarifa ya Wakili Mwasipu imeendelea kufafanua kuwa, wakati zoezi la kuandika maelezo hayo likiendelea alitokea askari mmoja ambaye bila kujitambulisha jina wala cheo chake, na bila kumueleza Wakili Madeleka kosa lake alimuita na kutaka kumuweka chini ya ulinzi, jambo lililoibua mabishano kati yao, na kwamba mabishano hayo yalichukua sura mpya pale Wakili Madeleka alipomshinikiza Afisa huyo wa Polisi kumuelezea kosa lake kwanza la sivyo hakubaliani na amri hiyo
Inaelezwa kuwa, baada ya muda Askari Polisi huyo alienda kushauriana na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam kwa faragha na ndipo baadaye walimuita Wakili Madeleka kwa pamoja na kumueleza kuwa kuna Wazungu wamefika kituoni hapo kulalamika wakidai kuwa walimpa Wakili Madeleka USD 2500 kwa ajili ya kesi yao, jambo ambalo Wakili Madeleka amelikanusha na kwamba hawatambui Wazungu hao
Baada ya majadiliano ya muda hatimaye Wakili Peter Madeleka akaruhusiwa kuendelea na zoezi lake alilokuwa analifanya awali ambalo ni kumsimamia mteja wake aliyekuja kutoa taarifa ya kuibiwa fedha Kariakoo huku akisubiri hatma yake kutoka kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam
Wakili Hekima Mwasipu ameieleza Jambo TV kuwa, kwa muktadha huo ni dhahiri kwamba muda wowote baada ya Wakili Peter Madeleka kumaliza kuandika maelezo hayo, huenda akawekwa chini ya ulinzi,
Jambo TV inaendelea kufuatilia undani wa suala hili.