Latest Posts

SAGAYIKA AWAKUMBUKA WANAFUNZI WENYE UHITAJI KALANGALALA

Diwani wa Kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika, leo Januari 10, 2026, amefanya ziara ya kutembelea Shule ya Msingi Kalangalala kwa lengo la kufuatilia zoezi la uandikishaji wa wanafunzi kwa muhula mpya wa masomo unaotarajiwa kuanza rasmi Januari 13, 2026.

Akiwa shuleni hapo, Sagayika ameeleza kuwa anatambua umuhimu mkubwa wa elimu kwa watoto, hivyo amepanga kufanya zoezi la kugawa vifaa vya shule kwa wanafunzi wenye uhitaji siku ya Jumatatu Januari 12, 2026. Amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika katika Ofisi ya Kata ya Kalangalala.

Aidha, Diwani huyo amebainisha kuwa ziara za kutembelea shule zilizopo ndani ya kata hiyo ni zoezi endelevu, ambalo linalenga kubaini changamoto mbalimbali zinazozikabili shule hizo ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Kata ya Kalangalala, Regina Comas Ketau, amesema kuwa kata hiyo ina jumla ya shule 9 za msingi, ambapo hadi sasa jumla ya wanafunzi 1,640 wamekwishasajiliwa. Ameongeza kuwa bado kuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la uandikishaji kwa asilimia 100.

Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalangalala, Mwalimu Sospter Luzige, amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kuandikishwa shuleni hapo, na kuacha kuwapeleka katika shule zisizo rasmi (za mitaani).

Kwa upande mwingine, Katibu wa Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kalangalala, Richard Nzagamba, amempongeza Diwani Sagayika kwa jitihada zake, hususan kwa kuwajali na kuwakumbuka wanafunzi wenye uhitaji wa msaada wa vifaa vya shule.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!