Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali shambulio dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, likikitaja tukio hilo kama la “kushtusha, kustajabisha, na linaloashiria kushindwa kwa vyombo vya usalama nchini.”
Padre Kitima alishambuliwa usiku wa Aprili 30, 2025, akiwa katika makazi ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam, na watu wasiojulikana. Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, kiongozi huyo wa kidini alijeruhiwa kichwani na kufikishwa hospitalini kwa matibabu.
Akizungumza kupitia taarifa rasmi ya chama hicho, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema tukio hilo ni la kutisha na linaibua maswali makubwa kuhusu hali ya usalama nchini.
“Inafikirisha, mtu wa kawaida anapata wapi ujasiri wa kumvamia na kumshambulia kiongozi wa dini aina ya Padre Kitima katika eneo lenye ulinzi wa kutosha kama TEC?” amehoji Semu.
“Shambulio la Padre Kitima ni ishara kuwa sasa hakuna aliye salama katika nchi yetu, na ni kiashiria cha kushindwa kwa mamlaka zenye wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi,” ameongeza.
ACT Wazalendo kimetaka uchunguzi wa haraka ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria. Aidha, chama hicho kimesema vitendo vya uvunjifu wa haki na mashambulizi ya aina hiyo vinahatarisha mshikamano na amani ya kitaifa.
“Tunahitaji kuona hatua za haraka zinachukuliwa. Vitendo vya namna hii vikomeshwe mara moja,” imeeleza taarifa hiyo.
Chama hicho pia kimetoa pole kwa Padre Kitima na kumtakia nafuu ya haraka, kikieleza kuwa mchango wake katika kutetea haki umeonekana na unaheshimiwa.