Latest Posts

SERIKALI: BILIONI 47 ZAMESHALIPWA KAMA MICHANGO YA WATUMISHI WA VYETI FEKI

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekanusha vikali taarifa zilizoandikwa na Gazeti la Rada la Aprili 14, 2025, zilizodai kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu malipo ya michango ya watumishi walioondolewa kwenye utumishi kwa kosa la kughushi vyeti hayajatekelezwa.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Aprili 15, 2025 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Mary Mwakapenda, serikali imeeleza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na zimekusudiwa kupotosha umma pamoja na kuichafua Ofisi ya Rais.

“Ofisi hii imesikitishwa na habari zilizoandikwa katika gazeti hilo kwani hazina ukweli na zimelenga kuwachafua viongozi, pamoja na kuleta taharuki kwa jamii,” amesema Mwakapenda.

Amesema kuwa maelekezo ya Rais yaliyotolewa Mei Mosi, 2022 jijini Dodoma yalielekeza kuwa watumishi waliotimuliwa kwa kosa la kughushi vyeti warejeshewe michango yao ya hifadhi ya jamii waliyochangia kupitia mifuko ya PSSSF na NSSF, jambo ambalo tayari limetekelezwa kwa ukamilifu.

“Tunapenda kuuthibitishia umma kuwa watumishi 15,288 waliotimuliwa kwa kosa la kughushi vyeti wameshalipwa jumla ya shilingi bilioni 47.02 kupitia mifuko ya PSSSF na NSSF kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais,” amesisitiza Mwakapenda.

Aidha, Ofisi hiyo imelaani kitendo cha gazeti hilo kuchapisha taarifa bila kuthibitisha ukweli wake kwa Mwanasheria wa ofisi hiyo kama ilivyoandikwa, hatua iliyotajwa kuwa ni kinyume cha misingi ya uandishi wa habari.

“Ni vyema vyombo vya habari vikazingatia maadili ya taaluma yao kwa kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa sahihi kwa umma,” ameongeza Mwakapenda.

Serikali imetoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizo potofu na kuendelea kuwa na imani na utendaji wa serikali katika kusimamia haki na maelekezo ya viongozi wa kitaifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!