Latest Posts

SERIKALI KUENDELEA KUWAUNGA MKONO WAVUVI NCHINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewataka wadau wa sekta ya uvuvi  barani Afrika kuifanyia kazi sekta ya uvuvi ili kuhakikisha inachangia kwenye pato la Taifa kwa kuhakikisha rasilimalizi za uvuvi zinalindwa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Jumatano Juni 05, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Wavuvi kufanyika barani Afrika sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya mafanikio ya sekta ya uvuvi, wenye lengo la kutathmini mwelekeo wa sekta ya uvuvi na kushirikisha  wadau mbalimbali, taasisi zinazowasaidia wavuvi wadogo zilizoko Afrika na kwingineko duniani.

“Nitoe wito kwenu wadau wa sekta ya uvuvi nchini kuhakikisha mnawapa kipaumbele wavuvi wadogo kwani ndio wanaochangia takribani asilimia 95 ya uvuvi wote Tanzania. Takwimu zinaonesha kuwa nchi ya Tanzania inazalisha wastani wa tani 475,579 za  samaki kati ya hizo, tani 429,168 zinatokana na uvuvi katika maji ya asili na kuchangia kiasi cha Shilingi trilioni 3.4” Amesema  Dkt. Biteko.

Aidha,  Dkt. Biteko amesema licha ya jitihada zinazochukuliwa kwenye sekta ya uvuvi Tanzania kama ilivyo kwa bara la Afrika, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo athari za mabadiliko ya tabia nchi, ushirikishwaji mdogo wa wadau katika usimamizi wa shughuli za uvuvi hususani wanawake na vijana pamoja na upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa ni heshima kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza Afrika wa wavuvi wadogo ambao chimbuko lake ni Mkutano wa Kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wavuvi Wadogo na Wafugaji Viumbe Kwenye Maji (IYAFA) uliofanyika Rome nchini Italia Machi, 2023.

Ameongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kutoa fursa kwa wavuvi wadogo kushiriki na kupaza sauti zao juu ya kuboresha uvuvi mdogo ikiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikishwaji wa wavuvi wadogo kwenye michakato ya uundwaji na utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, mipango na mikakati yote inayohusu wavuvi wadogo.  

 “Ni muhimu kusema kwamba uchaguzi wa Tanzania haukuwa kwa bahati, ila ni kwa kutambua umuhimu wa uvuvi mdogo kwenye nchi yetu na hatua ambazo nchi imechukua katika kuandaa na kutekeleza Mpango wa Nchi wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiyari wa Uvuvi Mdogo”, Amesema Ulega.

Amefafanua kuwa Kauli mbiu ya Mkutano huo ‘Muongo Mmoja wa Maendeleo: Kuongelea baadaye ya Uvuvi Mdogo Endelevu “ ilichaguliwa kutokana na kusherehekea miaka kumi ya utekelezaji wa Mwongozo wa Hiyari wa  Uvuvi Mdogo ili kufikia uvuvi mdogo endelevu na kwamba mkutano huu utafanya tathmini ya hali halisi ya utekelezaji wa mwongozo huo wa hiyari, sambamba na utekelezaji wa muundo wa kisera na Mkakati wa Mageuzi ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Afrika.

“Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuandaa mpango kazi wa kutekeleza mwongozo wa hiyari wa wavuvi wadogo ambapo katika mkutano huu tutapata fursa ya kueleza uzoefu wetu kwa nchi nyingine.” Amesisitiza Ulega.

 Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Mabadiliko ya Tabia Nchi kutoka nchini Malawi, Dkt. Michael Bizwick Usi amesema kuwa kupitia mkutano huo nchi wanachama wanapaswa kujadili masuala yanayohusu sekta ya uvuvi mdogo barani Afrika na kuangalia namna bora ya kuboresha kutokana na changamoto zilizopo.

Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Ang’ele Makombo N’tumba amesema kuwa kuna haja ya kuwasaidia wanawake katika sekta ya wavuvi wadogo na kuwa SADC kwa kushirikiana na wadau watasaidia nchi wanachama ili kuboresha sekta hiyo pamoja na kuzuia uvuvi haramu.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), Dkt. Tipo Nyabenyi Tito amesema licha ya kuwepo kwa changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo ikiwamo mabadiliko ya tabia nchi, FAO itashirikiana na wadau wa sekta ya wavuvi wadogo kwa kukuza uelewa na uwezo kwa wavuvi hao.

Kwa upande wake, Rais wa Mtandao wa Wavuvi Wadogo Barani Afrika, Gaoussou Gueye amesema kuwa sekta ya uvuvi mdogo ni muhimu hivyo inatakiwa kutumia vifaa vya kisasa ili kuongeza tija ya shughuli za uvuvi na kuwa wanawake wako katika sekta mbalimbali kuanzia ukusanyaji wa samaki hadi kuuza kwa walaji.

“Kama tunataka kusaidia uvuvi uwe endelevu lazima tuwe na mazingira wezeshi kwa wanawake ili kuleta usalama wa chakula katika bara la Afrika na utoshelevu wa chakula, katika uchumi wa buluu tunapaswa kulinda uchumi wetu kwa kukuza sekta kwa maendeleo ya Afrika.” Amesema Gueye.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!