Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imetangaza mpango kabambe wa kuimarisha ushirikiano na kuongeza uwekezaji ndani ya Puma Energy Tanzania, kampuni ambayo serikali inamiliki kwa usawa wa asilimia 50 pamoja na kampuni ya kimataifa ya Trafigura.
Tangazo hilo limetolewa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, siku ya Jumatatu mkoani Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa ngazi ya juu kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na uongozi wa kimataifa wa Puma Energy.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mark Russel, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Puma Energy Duniani, na Ben Ouattara, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Afrika. Ziara yao ya kikazi nchini Tanzania imekuwa ya kwanza kufanywa tangu uteuzi wao kushika nyadhifa hizo mapema mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo, Mchechu amesema kuwa serikali inaitazama Puma kama “kampuni ya kimkakati” ambayo inaweza kusaidia nchi hata pale panapotokea changamoto za kiuchumi au upatikanaji wa huduma muhimu.
“Kampuni hii, hata kama serikali ikipata changamoto za kifedha au kiutendaji, inaweza kutumika kama chombo cha kimkakati. Leo tumekubaliana kuongeza ushirikiano baina ya serikali na kampuni ya Trafigura kwa lengo la kuongeza uwekezaji, kupanua huduma, na kuzalisha faida maradufu kuliko sasa,” amesema Mchechu.
Amebainisha kuwa mipango ya muda mfupi na mrefu inahusisha kupanua mtandao wa huduma za mafuta na gesi, kuwekeza katika miundombinu ya CNG (Compressed Natural Gas), LPG (Liquefied Petroleum Gas- Gesi za kupikia majumbani) na kutumia kikamilifu rasilimali za nishati zilizopo nchini.
“Tunataka tuone kampuni hii ikizalisha mapato na faida mara mbili ya inavyofanya sasa. Tutapanua ‘distribution’, lakini pia tutaongeza bidhaa mpya kama CNG, LPG, na miradi ya LNG. Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za nishati — ni lazima tuzitumie kwa ufanisi zaidi kupitia kampuni kama Puma,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Duniani, Mark Russel, amesema kuwa baada ya kuteuliwa kuongoza kampuni hiyo mwezi Machi mwaka huu, ameona umuhimu wa kuitembelea Tanzania kwanza kwa sababu ni nchi ya kipekee katika mpango bora wa kibiashara wa kampuni hiyo barani Afrika.
“Nilipochukua nafasi hii, niliona wazi kwamba nchi ya kwanza kutembelea ni Tanzania. Umuhimu wake ni mkubwa mno — uhusiano mzuri wa kihistoria, nafasi ya kijiografia, na ukubwa wa biashara yetu hapa vinatufanya tuione kama nchi ya kipekee kwa ajili ya ukuaji wa muda mrefu,” amesema Russel.
Amesema kampuni hiyo iko katika mchakato wa kupitia upya mkakati wake wa maendeleo ili kuimarisha huduma kwa jamii kupitia mtandao wa vituo vya mafuta, kuongeza fursa za ajira, na kuchangia kwenye miradi ya nishati endelevu nchini.
Naye, Ben Ouattara, Mkurugenzi wa Puma Energy Afrika, amesema kuwa Tanzania inachukuliwa kama mshirika wa kimkakati wa muda mrefu wa kampuni hiyo, na kwamba kampuni inakusudia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara zake kwa Afrika Mashariki.
“Tunayo mipango ya kueneza biashara zetu kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine za ukanda huu. Lakini pia tunatambua kuwa ukuaji wa biashara lazima uambatane na ustawi wa jamii. Tunataka jamii inanufaika kwa huduma bora, ajira na miradi ya maendeleo kupitia uwepo wetu hapa,” amesema Ben.
Kwa upande wake, Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, ameeleza kuwa Tanzania inaongoza katika mchango wa mapato na faida kwa kampuni ya Puma barani Afrika. Amebainisha kuwa kampuni hiyo tayari imeanza utekelezaji wa miradi ya CNG na kupanua huduma za LPG katika mikoa mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa mwaka 2024 kampuni hiyo ilipata ongezeko la faida kwa asilimia 51, jambo linalothibitisha utendaji bora na kutoa matarajio ya gawio kubwa kwa serikali mwaka huu.