Latest Posts

SERIKALI WILAYA YA NJOMBE YAONYA WAANDIKISHAJI WA UCHAGUZI KUHUSU SIRI ZA MCHAKATO

News Njombe.

Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, serikali wilayani Njombe imewaonya waandikishaji wa vituo 227 vya uchaguzi kutotoa siri za mchakato wa uandikishaji, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kanuni za uchaguzi. Waandikishaji hao walikula kiapo cha utii na uadilifu kabla ya kuanza rasmi kazi yao.

Onyo hilo lilitolewa na Afisa Uchaguzi Msaidizi wa Wilaya ya Njombe, George Makacha, alipokuwa akiwaapisha waandikishaji hao kwenye ngazi za vijiji na kata, katika zoezi lililofanyika kwenye Kata ya Mtwango, wilayani humo.

“Yale utakayojua katika kazi hii hupaswi kumwambia mtu yeyote kwa sababu ni kazi ya siri. Ikiwa utaanza kuzungumza nje kuhusu mambo ya mchakato, tutakuwajibisha kwa mujibu wa kiapo ulichokula. Hili si kwa lengo la kutisha, lakini ni kuhakikisha mchakato unafanyika kwa usiri kama inavyotakiwa,” alisema Makacha.

Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, CPA Asha Msangi, aliwakumbusha waandikishaji kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa anapata nafasi ya kuandikishwa, bila ubaguzi.

“Tuna kata kumi na mbili kwenye halmashauri yetu, na tunategemea kuandikisha wapiga kura wasiopungua elfu hamsini na nne (54,000). Zoezi hili litaanza tarehe 11 na kukamilika tarehe 20 Oktoba 2024. Vituo vya kuandikisha vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni kwa siku zote kumi. Kila mwananchi anapaswa kujiandikisha akiwa na majina yake matatu, ambapo mwandikishaji atauliza majina, jinsia, umri, na mwisho atatia saini kwenye daftari la uandikishaji,” alisema CPA Msangi.

Baadhi ya waandikishaji waliokula kiapo, wakiwemo Wema Chilonwa na Andrea Mara, wamesema watazingatia maelekezo na kutekeleza kazi yao kwa uadilifu, huku wakiahidi kutunza siri za mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa viapo vyao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!