Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia fursa za Ununuzi wa Umma.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo maalum kwa watu wenye mahitaji maalum jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, amesema kuwa kuna upendeleo maalum wa kisheria unaolenga kuwawezesha makundi haya kunufaika na mikataba ya ununuzi wa umma.
“Serikali inatambua umuhimu wa makundi maalum katika kuchochea maendeleo ya taifa, hivyo tunataka kuona wanatumia fursa zilizopo kuchangia ukuaji wa uchumi,” amesema Simba.
Bw. Simba ameeleza kuwa hadi sasa, jumla ya vikundi 280 vya makundi maalum vimesajiliwa na kuhakiki taarifa zao katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST). Katika kipindi hiki:
Tuzo 440 za mikataba zimetolewa kwa makundi maalum zenye thamani ya Shilingi Bilioni 15; Vijana: Vikundi 163 (58%), Wanawake: Vikundi 96 (34%), Wenye Mahitaji Maalum (Walemavu): Vikundi 4 (2%), na Wazee: Vikundi 17 (6%).
Licha ya mafanikio hayo, Bw. Simba alikiri kuwa bado kuna muamko mdogo miongoni mwa watu wenye mahitaji maalum, hivyo PPRA imeanzisha mpango wa kuimarisha ushirikiano na taasisi kama TAB, TLB, Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuongeza usajili na ushiriki wa vikundi zaidi.
“Kila kikundi kinapaswa kuwa na watu kati ya watano hadi ishirini ili kistahili kushiriki katika fursa za ununuzi wa umma,” alifafanua.
Bw. Simba alisisitiza kuwa PPRA ina jukumu la kuhakikisha mifumo ya Ununuzi wa Umma inazingatia usawa, haki na uwazi, sambamba na kuendesha mafunzo ya kuhamasisha makundi maalum kujua na kutumia haki zao ipasavyo.
“Mafunzo haya ni mwanzo wa safari ya kuelewa haki zenu na kutumia fursa hizi kuboresha biashara zenu na kuongeza tija katika uchumi wa nchi.”
Akimpongeza washiriki, amesema ana matumaini kuwa maarifa watakayoyapata yatawasaidia katika shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania, Bw. Omary Itambu Amasi, aliishukuru PPRA kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu.
“Hapo awali tulikosa fursa kutokana na kukosa elimu. Leo PPRA mmetuletea ufunguo wa kufungua kila kitasa katika sekta ya ununuzi wa umma,” alisema Amasi kwa furaha.
Aliomba pia mafunzo haya yaendelezwe katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, huku akiomba bajeti za PPRA kuendelea kuwajumuisha watu wenye mahitaji maalum.