Latest Posts

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI KUPITIA MRADI WA VIWANDA WA KWALA

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amefanya ziara katika Kongani ya Viwanda ya Kwala (Sino-Tan) pamoja na Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuboresha miundombinu muhimu ya biashara na usafirishaji nchini. Ziara hiyo imehusisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, ikilenga kutoa taswira halisi ya maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya viwanda na bandari.

Mradi wa Kongani ya Viwanda ya Sino-Tan, unaotekelezwa katika eneo la Vigwaza, Kwala, ni mojawapo ya miradi ya kimkakati inayotarajiwa kubadilisha taswira ya viwanda nchini kwa kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo. Kongani hiyo inatarajiwa kuwa na viwanda 200 vya ukubwa wa kati na viwanda vidogo 300 vinavyoshughulikia sekta mbalimbali ikiwemo usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa vifaa vya ujenzi, uzalishaji wa dawa, viwanda vya nguo na viatu pamoja na viwanda vya kemikali. Hadi sasa, awamu ya kwanza ya mradi huo imekamilika kwa asilimia 80, huku miundombinu muhimu kama barabara, umeme na maji ikiwa tayari imeimarika ndani ya eneo la mradi ili kuwezesha shughuli za uzalishaji kuanza mara moja.

Hifadhi hii ya viwanda inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 100,000 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000, hivyo kuchochea uchumi wa taifa kwa kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hadi kufikia dola bilioni 6 za Kimarekani kwa mwaka. Aidha, mradi huo unakadiriwa kuongeza mapato ya kodi ya serikali kwa takribani shilingi trilioni 1.2 kila mwaka. Katika kuhakikisha uwekezaji huu unakuwa na tija kwa Watanzania, serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya msingi kama vile ujenzi wa barabara za zege, mtandao wa mawasiliano ya kasi kupitia fiber optic pamoja na usambazaji wa umeme na maji ili kutoa mazingira bora kwa wawekezaji.

Katika ziara hiyo, Msigwa ameeleza kuwa juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha sekta ya viwanda ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania. Ameeleza kuwa mradi wa Kwala utaongeza ufanisi wa sekta ya viwanda kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuimarisha biashara za kimataifa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kupitia taarifa yake mara baada ya ziara hiyo, kimeeleza kuwa maendeleo ya mradi huo yamepokelewa kwa matumaini makubwa na kwamba serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha uwekezaji huo unazaa matunda yanayotarajiwa kwa taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!