Latest Posts

SERIKALI YAOMBWA KUSHIRIKIANA NA WADAU KUBORESHA SHERIA YA NDOA KWA WATOTO

Baraza la Ulinzi wa Mtoto wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma limeitaka serikali kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sera na sheria ya ulinzi wa watoto ikiwamo sheria ya ndoa inayoruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuolewa ili kutokomeza ukatili dhidi yao.

Wito huo umetolewa Alhamisi Juni 20, 2024 na mwenyekiti wa baraza hilo Anthony Mlewa wakati wa  kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika  yaliyofanyika katika kijiji cha Kawawa kata ya Msanga wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma yaliyoandaliwa na Shirika Lisilo la Kiserikali Action Aid Tanzania, yenye kauli mbiu; Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.

Mlewa amesema ili kudhibiti ukatili unaoendelea dhidi ya watoto, jitihada za wadau wote na serikali ni muhimu kwa maendeleo endelevu na amewaomba wanajamii kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa dhidi ya ukatili kwa watoto.

Katika hatua nyingine Mlewa amebainisha changamoto inazowakabili ni ushirikishwaji duni kwenye masuala mbalimbali yanayohusu watoto na maamuzi, ukiukwaji wa haki za watoto na uhaba wa miundombinu shuleni na kutaka iboreshwe.

‘’Mimba za utotoni, ndoa za utotoni, vipigo vilivyopitiliza bado ni tatizo, pale penye haki wazazi wana wajibu wa kuhakikisha ulinzi wa mtoto ni kipaumbele siyo ombi, lakini pia wazazi wanawajibika kwenye masuala ya maadili kwa watoto” Amesema Mlewa.

Naye Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Yusuph Abdallah amesema kwa mujibu wa takwimu za wilaya ya Chamwino za Oktoba 2023-Juni 2024 kesi za ukatili zilizoripotiwa kituo cha polisi Chamwino zilikuwa 118 kati ya hizo wanaume ni 109, wanawake 9, watoto 26, na kesi 88 ziko mahakamani ambapo miongoni mwa kesi hizo ni pamoja na ubakaji, ukeketaji na vipigo.

Abdallah amewataka wazazi kutoa taarifa kwa dawati la jinsia endapo watapata taarifa za ukiukwaji wa haki za bindamu.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chamwino Obed Fredy amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwaachia watoto simu kwa muda mrefu ili kupunguza mmomonyoko wa maadili.

‘’Watoto wanajifunza matendo maovu kupitia mitandao ya kijamii hivyo niwaase wazazi kuwapeleka kwenye nyumba za ibada ikiwamo misikitini na makanisani ili waweze kujifunza maadili mema” Amesema Fredy.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Wadogo wilaya ya Chamwino (JUWACHA) lililopo chini ya Shirika Lisilo la Kiserikali Action Aid Tanzania Janeth Nyamayahasi amewataka wazazi kutenga muda kwa ajili ya malezi ya watoto kwa kushirikiana na viongozi wa dini, wazee wa kimila ili kupambana na mmonyoko wa maadili.

Clezensia Sahani kutoka shirika la Action Aid Tanzania amesema lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watoto ikiwa ni pamoja kupinga ukatili dhidi yao.

‘’Lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi ikiwamo elimu hata kama ni mlemavu, ukiangalia sasa hivi kuna mmonyoko wa maadili watoto wanajifunza kwa wazazi maana utandawazi unawaharibu, elimu wanayoipata iendane na maadili ya kitanzania,’’ Amesema Sahani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!