Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amewataka wanafunzi hususani wa kiume kutofumbia macho matendo yasiyo ya kawaida kama vile ulawiti na badala yake watoe taarifa kwa wazazi,walezi na walimu.
Hayo ameyazungumza Agosti 10,2024 kwenye bonanza la michezo lililo wakutanisha vijana kuelekea maadhimisho ya siku ya vijana Duniani iliyofanyika viwanja vya Chuo cha uwalimu kawaida (TTC) kilichopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Munkunda amesema kuwa kutokana na uwepo wa matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume ipo haja ya kuhakikisha wanatoa taarifa haraka kwa watu wa karibu ili kuweza kumsaidia mwenzao na kuweza kukomesha vitendo hivyo.
“Niwaombe sana watoto wangu wakiume msifumbie macho tabia mbaya, ukimuona mwenzako humuelewi mripoti kwa watu wa karibu tuweze kumsaidia, ukiona anakufata fata kila saa yuko karibu yako alafu ni mtoto wa kiume muulize lakini usimnyanyapae tutoe taarifa ili tuweze kumsaidia kwasababu inawezekana ameshapata changamoto anahitaji msaada.”Amesema Munkunda
Benson Daud Mratibu wa Bonanza la Michezo kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Global Peace Foundation lililopo mkoani Mtwara, amesema lengo la kuandaa bonanza hilo ni kuwakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali na kuwahamasisha kutumia teknolojia vizuri ili iwe faida na kuwapatia maendeleo.
Pia kuonesha suluhisho mbalimbali za vijana zinazozingatia dijitali na ubunifu katika ulimwengu kwa viwango vinavyochangia maendeleo endelevu.
Hata hivyo amewataka vijana hao kuwa mstari wa mbele kutumia dijitali kwa faida na kuacha matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Joseph Michael mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu kutoka shule ya sekondari Mtwara Ufundi iliyopo kwenye Manispaa hiyo, ameiomba serikali kutafuta mbinu ambayo itawasaidia walemavu kupata nafasi ya kujua mambo ya teknolojia na kuwawezesha kufaulu zaidi.
“Mfano sisi watu wenye ulemavu wa macho tunaweza tukatengenezewa vifaa vikatusaidia vile wanavyotufundisha walimu tukaweza kuelewa na kufaulu na sisi tujione watu wa kawaida.”Amesema Michael
Bonanza hilo la michezo lenye kauli mbiu isemayo ‘Vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo endelevu’ limewakutanisha vijana zaidi ya 1,500 kutoka shule mbalimbali za sekondari wilayani humo ikiwemo Shangani, Sino na Mtwara ufundi.