Serikali imeombwa kuwekeza kwenye utalii wa ndani kwa kuanzisha bodi ndogo ya utalii ya mkoa ili iweze kupanga na kusimamia mikakati ya utalii kwa pamoja, jambo litakalosaidia Mkoa wa Mtwara kukua katika sekta hiyo.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Tamasha la Nyangumi Festival, Mkurugenzi wa Visit Mtwara Samir Murji, amesisitiza kuwa serikali inapaswa kuweka nguvu zaidi kwenye utangazaji kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye maonyesho ya utalii ya kitaifa na kimataifa ili kuwakilisha utalii wa Mtwara.
Ameongeza kuwa ni muhimu kutoa elimu mashuleni na kwa jamii kuhusu vivutio vilivyopo kama vile nyangumi na akiba pori ya Rumesule, pamoja na kuweka ramani ya vivutio vyote vya utalii vinavyopatikana kwenye mkoa huo ambavyo bado havijulikani, hatua itakayosaidia vivutio hivyo kutangazwa kitaifa na kimataifa na kuomba kuongeza ushirikiano ili sekta hiyo izidi kukuwa na kuongeza mapato, ajira na maendeleo katika jamii.
Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma Amos Singo,amesema tamasha hilo lina malengo mahususi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii wa bahari na kuutangaza mkoa kitaifa na kimataifa, kuongeza uelewa juu ya uhifadhi wa bahari na viumbe wake hasa nyangumi ambao ni kiashiria cha afya ya mazingira ya bahari.
Ameeleza pia kuwa tamasha hilo linatoa fursa kwa wananchi hususan vijana na wanawake kunufaika kiuchumi kupitia huduma mbalimbali kama utalii, malazi, vyakula, sanaa na usafirishaji ambapo kupitia ushirikiano uliopo kati ya serikali, sekta binafsi, jamii za pwani na wadau wengine wa maendeleo, tamasha hilo litaendelea kukua na kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya Mtwara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya ametaja baadhi ya vivutio vinavyopatikana mkoani humo ikiwemo misitu ya asili aina ya mikoko, hifadhi tengefu za wanyamapori za Lukwika Lumesule na Msanjesi katika wilaya za Masasi na Nanyumbu, mji mkongwe wa Mikindani, pamoja na fukwe nzuri za Msimbati na Msangamkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Ameongeza kuwa matamasha kama la Nyangumi Festival yatasaidia kutekeleza falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifungua nchi,Rais alisisitiza kuwa watumishi katika maeneo yao ya usimamizi wahakikishe wanaweka mipango madhubuti ya kuwavutia wawekezaji na watalii kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameiomba serikali kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia wananchi kushiriki kikamilifu kwenye matamasha mbalimbali ya utalii ikiwemo Tamasha la Nyangumi, kuanzia kwenye ufunguzi hadi kumuona nyangumi, ili waweze kujifunza na kumjua zaidi. Wameomba pia elimu iendelee kutolewa kuhusu utalii uliopo mkoani na faida ya vivutio hivyo.