Latest Posts

SERIKALI YAONYA WATUMISHI WA UMMA WANAOFANYA KAZI KWA MAZOEA

Serikali imeweka msimamo mkali dhidi ya Watumishi wa Umma wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, hali inayosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kushindwa kupata huduma bora.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ametoa kauli hiyo wakati wa kikao kazi na Watumishi wa Manispaa ya Tabora, ambapo amewasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

Sangu ameeleza kuwa tabia hiyo ya kufanya kazi kwa mazoea inakwaza jitihada za Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo katika ofisi za Serikali. Amekumbusha watumishi hao kuwa kutoa huduma bora kwa wananchi siyo hisani, bali ni wajibu wao wa kisheria.

Katika hatua nyingine, Sangu alizitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuhakikisha haki na stahiki zote za watumishi zinasimamiwa kwa usahihi. Ameonya dhidi ya tabia ya baadhi ya viongozi kutoa ushauri usiofaa kwa nia ya kuwafurahisha viongozi wa juu, hali ambayo inaweza kuwaumiza watumishi.

Sangu ameeleza kuwa ni aibu kuona watumishi wakiwasilisha changamoto zao kwa viongozi wa kitaifa wanapofanya ziara, wakati masuala hayo yanapaswa kutatuliwa kwenye ngazi ya wilaya au mkoa. Amesema kitendo hicho kinadhihirisha kuwa baadhi ya watumishi hawawajibiki ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao.

“Si jambo la kupendeza kuona watumishi wanatumia muda wa kazi vibaya kwa kupiga soga na kutumia simu,” amesema Sangu.

Sambamba na hilo, Sangu ametoa angalizo kwa watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vitakavyowapelekea kufukuzwa kazi, huku akisisitiza kuwa kurudi kwenye utumishi wa umma ni mchakato mgumu na wa muda mrefu.

Amewasihi watumishi kutimiza wajibu wao kwa umakini ili kuepuka matatizo yanayoweza kusababisha kuondolewa kazini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!