Serikali imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ugele, Manispaa ya Iringa mkoani Iringa ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hususan akina mama wajawazito.
Wananchi wa kijiji hicho wameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya, ikiwalazimu kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma katika kata za jirani. Gharama za usafiri zimekuwa mzigo kwao, jambo ambalo limeathiri upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakati.
Katika ziara yake ya mtaa kwa mtaa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kusisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unakamilika ndani ya mwezi mmoja. Amesihi wananchi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa zahanati hiyo ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa ufanisi na kuboresha ustawi wa jamii.