Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema serikali imetoa shilingi bilioni 114.5 ndani ya kipindi cha miaka mitatu kwa mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu mkoani humo.
Mkuu wa mkoa huyo ameyasema hayo katika kilelele cha kuadhimisha wiki ya elimu mkoani humo.
Kanali Sawala amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 76.6 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shilingi bilioni 37.9 kwa ajili ya kugharamia elimu ya msingi bila malipo.
Ameongeza kuwa kutokana na fedha hizo na mikakati ya mkoa ya kuboresha elimu ambayo iliwekwa na mkoa, mkoa huo umeweza kuboresha elimu na kuleta mafanikio kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ufaulu kuongezeka.
“Moja ya mikakati ambayo iliwekwa na mkoa ni kuanzisha juma la elimu kwa lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya elimu katika mkoa, kutoa motisha kwa walimu, wanafunzi na Halmashauri pamoja na wadau wa elimu” Amesema.
Akitaja baadhi ya maendeleo ya elimu yaliyopatikana Mkoani Mtwara, Afisa Elimu wa Mkoa John Lupenza ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa ni ufaulu wa wanafunzi ambao wanajiunga na shule za sekondari, kuongeza uwezo wa wanafunzi wa darasala la kusoma, kuandika na kuhesabu.
Katika hafla ya kuhitimisha juma la elimu, serikali ya mkoa imetoa zawadi mbalimbali ikiwa pamoja na baiskeli, pikipiki, pesa taslimu na kompyuta ambayo imetolewa kama motisha kwa walimu, wanafunzi, wakurugenzi wa halmashauri na wadau ambao wamekuwa wakisaidia mkoa huo katika kuboresha mazingira ya elimu.
Halikadhalika Kanali Sawala amekabidhi tuzo ya shukrani kwa mdau wa elimu na mgeni maalumu Meja Jenerali Marko Elisha Gaguti ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara miaka miwili iliyopita kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kukuza sekta ya elimu mkoani Mtwara.