Serikali ya Tanzania imewahimiza wadau wa maendeleo kuunga mkono jitihada zake za kukuza sekta za kilimo na viwanda vya uzalishaji huku ikirejea namna nchi zilizoendelea zilivyopitia mapinduzi katika sekta hizo kutokana na mchango mkubwa wa wadau wa maendeleo wa nchi hizo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo katika mazungumzo kati ya serikali na wadau hao jijini Dodoma ambapo amewaalika kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye kilimo na viwanda vya kuongeza thamani.
Ameongeza kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, hivyo kukuza sekta za uzalishaji na ajira ni kipaumbele muhimu.
“Elimu na viwanda vya uzalishaji vitakuwa msingi wa mipango na utekelezaji wa shughuli za kiuchumi katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ili kuzalisha ajira kwa vijana hawa”, amesema Prof. Kitila.
Aidha Prof. Kitila amebainisha kuwa serikali imefanya maboresho ya kisera na kisheria ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.