Latest Posts

SGR YA MIZIGO KUPUNGUZA GHARAMA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uzinduzi rasmi wa safari za mizigo kwa kutumia reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ni hatua ya kihistoria ambayo itaongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza siku ya Alhamisi wakati wa hafla ya uzinduzi huo katika eneo la Kwala, mkoani Pwani, Rais Samia amesema Tanzania imeamua kwa dhati kuimarisha mifumo yote ya usafirishaji- barabara, anga, maji, na sasa reli ili kukuza uchumi na kulinda mazingira.

“Ndugu wananchi, uzinduzi wa safari za mizigo kwa kutumia reli ya kisasa ya SGR ni ushahidi kuwa Tanzania imeamua kwa dhati kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo. Reli ya SGR kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama ya usafirishaji, uchakavu wa barabara na uharibifu wa mazingira,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameeleza kuwa kwa kutumia reli ya SGR, mizigo kutoka bandarini inaweza kufika Kwala ndani ya dakika 45 hadi saa moja, na kufika Dodoma ndani ya saa nne hadi tano ikilinganishwa na wastani wa saa 30 hadi 35 zinazotumika na magari ya mizigo kwa safari hizo kwa sasa.

Ameongeza kuwa kwa sasa, magari ya mizigo hutumia hadi saa 24 hadi 30 kukamilisha taratibu bandarini kabla ya kuanza safari- muda ambao utapunguzwa kwa kiasi kikubwa kupitia mfumo wa kisasa wa reli ya SGR.

Rais Samia amewataka Watanzania kuutumia mradi huo kama kichocheo cha maendeleo na uthibitisho kuwa taifa linaendelea kupiga hatua.

Uzinduzi huo pia uliambatana na kuwekwa kwa jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda Kwala na kuzinduliwa kwa Kituo cha Kimataifa cha Lojistiki cha Kwala, hatua zinazolenga kujenga mfumo jumuishi wa usafirishaji na utengenezaji wa bidhaa nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!