Na; mwandishi wetu
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu imeendelea tena leo, Alhamisi Februari 19.2026, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ambapo mashahidi mbalimbali wa Jamhuri wameendelea kutoa ushahidi wao Mahakamani hapo
Kesi hiyo Na. 19605/2025 inayosikilizwa mfululizo mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, awali imeshuhudiwa Mahakamani hapo Askari Polisi mpelelezi H. 937 Detective Koplo Vicent akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka
Shahidi wa pili (2) kwa siku ya leo kutoa ushahidi wake, ambaye ni shahidi wa 13 kwa ujumla wake katika muendelezo wa mashahidi wa Jamhuri ni shahidi wa siri (P3), shahidi huyu ametoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzengeli
Akiwa chini ya kiapo kama ilivyo ada, P3 ameieleza Mahakama kuwa yeye ana umri wa miaka 35, Dini yake ni Muislamu, na kwa takribani miaka minane (8) sasa amekuwa akijishughulisha na uendeshaji wa Bodaboda
Shahidi huyu ambaye ameieleza Mahakama kuwa ni Mkazi wa Mtaa wa Mtengule, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, amesema yeye ni mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzia mwaka 2021 mpaka sasa, na kwa muda wote huo amekuwa akishiriki kikamilifu matukio na shughuli mbalimbali za chama hicho zinazofanyika mkoani Mbeya
Anasema anakumbuka mwaka 2024 alishiriki kwenye maandamano ya CHADEMA yaliyofanyika Mbeya, ambapo yeye alishiriki kwenye msafara wa maandamano uliioongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa wa wakati huo Freeman Mbowe
Tukio lingine analokumbuka linalohusiana na CHADEMA ni kongamano lililoandaliwa la vijana (BAVICHA) lililopaswa kufanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda -Nzovwe, lakini kwa bahati mbaya kwao kongamano hilo halikufanyika kwa sababu serikali ililizuia
Anasema tarehe 04/04/2025 akiwa kijiweni kwake anakopaki Bodaboda, akiwa na simu yake ya mkononi, alikuwa anaperuzi mitandaoni akabahatika kuona hotuba fupi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa wa sasa Tundu Lissu akiwa anahutubia, na kwamba kupitia hotuba hiyo alizungumzia mipango ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
Anaeleza kuwa, hotuba hiyo aliiona katika mtandao wa kijamii wa Youtube ambapo mhutubiaji (Tundu Lissu)Â alimfahamu kwa haraka, kwakuwa kwa muda mrefu amekuwa akimfahamu Lissu kupitia mitandao ya kijamii, na hiyo ni baada ya kuwa mfuatiliaji sana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tangu mwaka 2021
P3 ameieleza Mahakama kuwa anafahamu kuwa Tundu Lissu ndiye Mwenyekiti wake wa chama Taifa kwa sasa, ambapo baada ya kuwa amesikiliza zile video YouTube, ambapo baada ya kusikiliza, kuelewa na kuridhika nayo yale anayozungumza akajaribu kuongea na wenzake kuwashawishi kile anachokitaka Mwenyekiti wake wa Taifa waungane, wawe kitu kimoja kupambana na kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
Alipoulizwa kuzuia uchaguzi kwa namna gani, shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa uzuiaji wake ungeenda sambamba na kuwafanyia vurugu wanaokwenda kupiga kura, ikiwemo na kuwapiga mawe
Ameeleza kuwa mambo hayo ya ushawishi alikua anafanyia kwenye kijiwe chake cha bodaboda, na kwamba kuna baadhi ya wale aliokuwanao kijiweni waliridhika na kukubali kuunganae na wengine hawakuridhika, na hivyo makundi hayo mawili (walioridhika na wasioridhika) wote wakaendelea na mambo yao
Anasema baada ya muda akatokea mtu mmoja akamwambia ‘Braza naomba njoo tuongee kidogo, waliposogea pembeni yule mtu akajitambulisha kuwa yeye ni Afisa wa Polisi akamwambia waende Kituo cha Polisi kwa mahojiano
Shahidi huyo wa siri (P3) amedai Mahakamani hapo kuwa alipofika Kituo cha Polisi aliambiwa akae chini, atoe viatu, mkanda na kila kitu alichokuwa nacho akakabidhi mapokezi pale kituoni na yeye akapelekwa mahabusu
Amedai kuwa, baada ya kukaa mahabusu kwa muda mfupi, kisha akapelekwa kwenye chumba cha mahojiano, ambapo akiwa huko alihoji kwanini alikuwa anahamasisha kufanya uasi wa kwenda kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025?
Anasema baada ya mahojiano akaambiwa atafute mtu au watu wa kumdhamini ambapo alikuja ndugu yake akamdhamini lakini akaambiwa kila baada siku tatu (3) awe anaenda kuripoti kituoni hapo
Alipoulizwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzengeli kuhusu siku ya tarehe 17/04/2025 kwamba anakumbuka nini?, shahidi huyo amesema akiwa njiani kuelekea kijiweni kwake alipigiwa simu ya kumtaka akaripoti Kituo cha Polisi Ilomba, alipofika akakutana na askari aliyemuandika maelezo mwanzo anaitwa Amani akahojiwa tena alipomaliza akasaini, na yeye akaambiwa aendelee na utaratibu wa kuripoti kila baada ya siku tatu (3) kama alivyokuwa anafanya

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake Mahakamani, baadae Mahakama ilimpatia nafasi mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kuhoji maswali ya dodoso (Cross Examination), na hapo ilikuwa hivi:
Lissu: Hapo ulipo unanion?
Shahidi: Sikuoni
Lissu:.Shahidi waeleze Majaji mfuasi wa CHADEMA anakua na kitambulisho gani
Shahidi: Nakusikia
Lissu: Jibu swali
Shahidi: Hawi na kitambulisho kwa sababu si mwanachama
Lissu: Mimi Mwenyekiti wa CHADEMA au kiongozi mwingine wa CHADEMA ambae yupo hapa, na huna kitambulisho atajuaje kama wewe ni mfuasi ws CHADEMA?
Shahidi: Mimi ni mfuasi wa CHADEMA
Lissu: Kuna namna yeyote naweza nikajua?
Shahidi: Kujua huwezi inabidi uwe na imani
Lissu: Sio suala la imani, hapa tuko kwa Kaisari, hakuna namna yoyote mimi kuthibitisha, kweli au si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze majaji kama wafuasi wa CHADEMA huwa wanaorodheshwa mahali ili wajukikane
Shahidi: Sijajua wanaorodheshwa wapi?
Lissu: Waeleze Majaji kama wafuasi wa CHADEMA huwa kuna mahali wanaenda kujitambulisha
Shahidi: Hakuna mahali wanaenda kujitambulisha
Lissu: Waeleze Majaji kama nilichoksoma ndicho kilichoandikwa kwenye maelezo yako
Shahidi: Ndio, ndicho
Lissu alimsomea shahidi maelezo aliyoandika akiwa Kituo cha Polisi tarehe 17/04/2025 huku akimuomba maelezo hayo yakabidhiwe Mahakamani kama kielelezo cha ushahidi, hatimaye Mahakama ilipokea kielelezo hicho na kukipa jina la D12
Lissu: Shahidi waeleze Waheshimiwa Majaji kama katika maelezo yako hayo kuna mahali kumeandikwa kutawanywa uwanjani
Shahidi: Mwaka 2024 nilijiandaa kushiriki kongamano la vijana lakini lilishindwa kufanyika kwa sababu lilizuiliwa na serikali
Lissu: Waeleze Majaji sehemu ambapo umeandikaa kutawanywa, yapo hayapo?
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema hilo kongamano kwa bahati mbaya au nzuri halikufanyika
Shahidi: Kweli
Lissu: Kwa hiyo mfuasi wa CHADEMA kongamano halikufanyika kwako ni bahati nzuri?
Shahidi: Mi sijui
Lissu: Najuaje kama wewe sio pandikizi la Polisi?
Shahidi: Naomba kama tunaendelea na swali lingine, tuendelee
Lissu: Tarehe 04/04/2025 umesema ukiwa kijiweni ukiwa na simu yako
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye maelezo yako kuna mahali umesema ulikuwa na simu
Shahidi: Nakumbuka kwamba tarehe 04/04/2025 nikiwa nafuatilia taatifa kwenye mtandao wa Youtube nilikua na simu yangu
Lissu: Hayo maneno yapo kwenye karatasi?
Shahidi: Hayajaandikwa
Lissu: Waeleze Majaji kama unafahamu kuwa unaweza kufuatilia YouTube kwenye Kompyuta?
Shahidi: Mimi siwezi
Lissu: Inawezekana au haiwezekani?
Shahidi: Mimi binafsi kwenye Kompyuta sio mzoefu
Lissu: Waeleze Majaji kama unaweza kufuatilia mtandao wa YouTube kwenye Televisheni
Shahidi: sijui
Lissu: Shahidi umesema hivi siku hiyo uliona video fupi iliyokuwa inamuonyesha Mheshimiwa Tundu lissu akizungumza kuzuia uchaguzi mkuu, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Kuna mashahidi wamesema ile video ina masaa mengi
Shahidi: Ndio
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna sehemu umeeleza juu ya urefu ws hiyo video
Shahidi:…
Lissu: Umeeleza baada ya kuona hiyo video ukahamasisha vijana wenzako, na baada ya ushawishi huo mtu mmoja alitokea akakuita pembeni, waeleze Majaji kama hayo maneno yapo kwenye maelezo yako
Shahidi: Napitia kidoogo
Lissu: Umesema niliposogea pembeni akajitambulisha kuwa ni askari Polisi akaniambia twende kituoni, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama hayo maneno yapo kwenye ushahidi wako
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema kwenye mahojiano alikuuliza kwa nini unahamasisha uasi?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama hayo maneno yapo
Shahidi:.Hapana
Lissu: Umesema alikuambia uendelee kuripoti kila baada ya siku tatu,.hayo maneno yapo au hayapo?
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema wewe ni dereva bodaboda, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama umeonyesha leseni yako ya udereva bodaboda
Shahidi: walipochukua, walithibitisha
Lissu: Nimeuliza umeonyesha Majaji leseni yako?
Shahidi: Hapana
Lissu: Bodaboda ni Pikipiki
Shahidi: sahihi
Lissu: Umewaeleza Majaji juu ya namba ya hiyo Pikipiki yako?
Shahidi: Hapana
Lissu: Pikipiki ina kadi yake inayotolewa na TRA, umewaonyesha Majaji kadi ya hiyo Pikipiki?
Shahidi: Mimi sio mmiliki
Lissu: Swali langu, umeionyesha kwa Majaji?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kijiwe chako hatukijui, leseni hatujaona, namba ya Pikipiki, kadi hujaileta waeleze Majaji kuna uwezekano wa mtu yeyote kuthibitisha kuwa wewe ni dereva bodaboda?
Shahidi: Mimi sijui
Lissu: Umesema katika kielelezo kwamba umeshiriki shughuli mbalimbali za CHADEMA ambapo ulikuwa kundi la Mwenyekiti Freeman Mbowe
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna sehemu uliandikisha jina lako kwenye orodha
Shahidi: Hapana
Lissu: UlijitambulIsha kwa kiongozi yeyote kwenye hayo maandamano?
Shahidi: Sikuweza ila baadhi ya wafuasi wenzangu walijua
Lissu: Umewataja?
Shahidi: Hapana
Lissu: Ulipigwa hata picha tu?
Shahidi: Sijui
Lissu: Tunajuaje kama ulijiandaa kushiriki? ulijiandikisha kwa BAVICHA Mbeya?
Shahidi: Sijui
Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, watathitbitishaje kama wewe ulikuwa kwenye mkutano wangu
Shahidi: Mimi najua kwamba ni mfuasi wako na kama unanikataa sawa
Lissu: Sikukatai, naogopa wasiojulikana, kama wewe
Shahidi: Mimi ni mfuasi wako
Lissu: Ila unashirikiana na mapolisi kuwasaidia kutoa ushahidi wa kwamba mimi ni mhaini?
Shahidi: Hilo mi sijui, Nimekujibu maswali yako
Lissu: Waeleze Majaji kama umeeleza majina ya vijana wenzako uliokuwa unawashawishi
Shahidi: hili siwezi kuwataja na sijawataja
Lissu: Uamuzi wa kwamba utaenda kupiga watu mawe ni uamuzi wako
Shahidi: Kutokana na hamasa yako
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna sehemu ambayo Mwenyekiti alituambia tukapige watu mawe
Shahidi: Hayapo
Lissu: Kuna mahali popote kwenye maelezo yako umesema kwamba Mwenyekiti Tundu Lissu alisema tukafanye vurugu?
Shahidi: Kitendo cha kuhamasisha kuzuia uchaguzi tayari ni vurugu
Lissu: Yapo au hayapo
Shahidi: Hayapo
Lissu: Unafahamu maana ya neno uasi?
Shahidi: Hapana
Lissu: (Anamsomea shahidi maana ya uasi) kitendo cha uvunjaji wa sheria kinachofanywa na kikundi cha watu kwa lengo la kubaini mfumo wa kisiasa wa nchi yao
Shahidi:
Lissu: Mtu akisema anahamasisha uasi kama kitendo cha aina hiyo kuvunja sheria ili kubadilisha serikali iliyopo ni uhaini?
Shahidi: Hapo mi sijui
Lissu: Waeleze Majaji kama kuwapinga wenye mamlaka ni uhaini
Shahidi: Sijui
Lissu: Sheria ya Uchaguzi 2024 hakuna sehemu inasema kuzuia uchaguzi ni kosa la jinai
Shahidi: Sijui
Lissu: Waeleze Majaji hilo shtaka, tuhuma dhidi yako iliishia wapi?
Shahidi: Niliripoti mpaka tarehe 04/09/2025 nikaambiwa nisubiri nitapigiwa simu na nikaja kupigiwa simu nije kutoa ushahidi Mahakamani
Lissu: Waeleze Majaji kama umefunguliwa mashtaka ya jinai ya kula njama, kipiga watu mawe kufanya vurugu
Shahidi:…
Lissu:.Ulikula njama na mapolisi uwe pandikizi CHADEMA ili uje utoe ushahidi hapa?
Shahidi: sijui
Lissu: Ulipataje taarifa kuja Mahakamani?
Shahidi: Nilipigiwa simu, nikapewa summons
Lissu: Nani alikulipia nauli?
Shahidi: Nilijilipia mwenyewe
Lissu: Hapa unaishi hotelini au wapi?
Shahidi: nimefikia gesti
Lissu: Waeleze Majaji nani anaelipia gesti?
Shahidi: Mimi mwenyewe
Lissu: Kwa hiyo umekuja hapa kutoka Mbeya kwa kujitolea kama raia mwema?
Shahidi: Ndio
Pamoja na maswali mengine shahidi P3 alikiri kuwa hakuwahi kutishiwa japokuwa amedai kwenye jamii vitisho vipo, baada ya Lissu kuhitimisha maswali ya dodoso (Cross Examination) Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzengeli alimuuliza shahidi maswali ya kusawazisha (Re-examination) kutokana na yale aliyoyajibu alipoulizwa na Lissu
Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzegeli alimtaka shahidi kusoma mstari wa tatu (3) katika aya ya mwisho ya maelezo yake shahidi alisoma, “wakati tunaendelea kubishana alifika mtu aliyejitambulisha kama askari polisi”
Wakili huyo alimtaka shahidi kufafanua kuhusu alipoulizwa kama kulikuwa na maneno yanaeleza kufanya vurugu shahidi alidai ndiyo,
Hata hivyo, mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo alisimama na kuwaeleza Majaji kuwa hakumuuliza shahidi aeleze uhusiano kati ya kufanya vurugu na kuzuia uchaguzi bali alimuuliza kama hayo maneno kufanya vurugu yapo kwenye maelezo yake, hivyo kutoa rai kwa Mahakama kuwa endapo itaruhusu kufanya hivyo nitaomba kudodosa kwenye hilo.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, shahidi mwingine wa tatu (3) kwa siku ya leo na wa 14 katika orodha ya mfululizo wa mashahidi wa Jamhuri akaanza kutoa ushahidi wake
Huyu pia ni shahidi wa siri (P9), ambaye amejitambulisha kuwa ana amri wa miaka 38, fundi Umeme, Mkazi wa Mbeya, yeye ametoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Cuthbert Mbilingi
Shahidi huyo ataendelea kesho, kwa mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kuanza kumuhoji shahidi huyo (P9) maswali ya dodoso (Cross Examination).