Na; mwandishi wetu
Jina la Sheikh Abeid Amani Karume katu haliwezi kufutika masikioni kama sio kwenye moyo ya Watanzania, sio tu kwa sababu aliongoza Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 lakini pia huyu ni muasisi mwenza wa Muungano wa Tanzania unaotokana na nchi mbili (2) huru yaani iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo ziliungana na kuunda Taifa moja huru la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Hilo pekee, halihitaji kufungua kitabu chote cha maisha ya Sheikh Abeid Amani Karume ili kujuwa kwa namna gani vitabu vya historia vya Tanzania, Afrika kama sio ulimwengu kwa ujumla wake vitaendelea kumuandika, kusimulia, kufundisha hadi mwisho wa maisha yetu hapa Duniani, na huo ndio uhalisia ambao hauwezi kufutika
Umoja, uzalendo, urafiki na ushirikiano wake wa karibu na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika (sasa Tanzania Bara), ambaye baada ya Muungano alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sio tu wa kupigiwa mfano na kuigwa, bali ndio msingi wa amani yetu, umoja wetu, muungano wetu na salama yetu; historia za watu hawa wawili na urafiki wao ni ndefu sana na katu ni ngumu kuweza kusimulia kwa dakika, saa, siku, miezi au miaka badala yake kila anayetoka hadharani kufundisha, kusimulia au kusoma ni dhahiri anatoa sehemu ndogo ya uelewa wake kuhusu miamba hiyo ya Afrika iliyotangulia mbele za haki ikituachia nchi moja, ingawa leo nitamuangaza zaidi Sheikh Abeid Amani Karume, ingawa hapa naendelea kusisitiza kuwa ni kwa uchache sana kutokana na uelewa wangu
Ndio, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kama nilivyokujuza hapo awali alikuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, aliyezaliwa mwaka 1905 na kufariki Aprili 07.1972, kifo kilichotokana na kupigwa kwa risasi akiwa kwenye makao ya ofisi za Afro Shiraz Party wakati huo (sasa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui) Zanzibar
Hayati Sheikh Abeid Amani Karume alishika hatamu ya kuiongoza Zanzibar baada ya mapinduzi matukufu yaliyomwangusha Sultani aliyekuwa akitawala Zanzibar hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 1964, miezi mitatu baada ya mapinduzi hayo ndipo Zanzibar ilipoungana na Tanganyika ambapo kufuatia muungano huo, kwa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Rais wa Tanzania, basi moja kwa moja Sheikh Karume alikuwa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania (ikumbukwe kuwa kipindi hicho serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa na Makamu wa wawili wa Rais, ambapo kwa mujibu wa Katiba kipindi hicho ilieleza wazi kuwa anayekuwa Rais wa Zanzibar ndiye anayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa JMT)
Inaelezwa kuwa, simulizi za maisha ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume zimekuwa za ‘utata’, kwa mfano wapo wanaosema kuwa alizaliwa eneo la Kiongoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar na mama yake ni Amina Kadir (Kadudu) na kuwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano (5) wa bwana Amani Karume, lakini pia wapo wanaodai kuwa alitokea nchini Malawi na kufika Visiwani Zanzibar akiwa mdogo na wengine wakidai kuwa wazazi wake walitokea ile iliyokuwa ikiitwa Rwanda-Urundi (sasa ni nchi za Rwanda na Burundi)
Hata hivyo, taarifa hizo zilizowahi kuandikwa na vyombo mbalimbali vya habari ulimwenguni kote likiwemo gazeti maarufu la Marekani la ‘Jewish Week’ ambalo limewahi kukiri kwenye moja ya makala zake kuwa halina uthibitisho wa moja kwa moja wa maisha ya asili ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, hivyo ni ukweli kwamba yote yanayosemwa yanabaki kuwa ni maneno ya watu, na kwa sisi Watanzania tunapaswa kufuata kile kilichoandikwa kwenye vitabu vyetu vya historia na si vinginevyo
Katika moja ya makala zilizowahi kuchapishwa na gazeti maarufu la hapa nchini la ‘Mwananchi’, makala ambayo iliandikwa na mwandishi mkongwe kabisa hapa nchini Salim Saidi Salim, kupitia makala hiyo Salim anasema mke wa mwanzo wa Mzee Karume aliyemjuwa kwa karibu ni Fatma Gulamhussein (mama Fatma Karume) na hiyo ni tokea alipoanza kupata fahamu zake mwanzoni mwa miaka ya 1950
Salim anasema alimuona Hayati Sheikh Karume kuwa ni rafiki wa kila mtu mtaani licha ya tofauti za kisiasa, lakini zaidi ni kwa watoto ambao walipenda kuazima baiskeli yake, yeye Salim akiwa mmoja wao
Inaelezwa Sheikh Karume kila alipokutana na mtoto wa kiume yeyote yule yeye alimuita ‘Shabbab’ na wa kike ‘mchumba wangu’, ambapo katika hilo Salim anasema bahati mbaya kwake licha ya kukaanae mara nyingi na licha ya kwamba alimfundisha karata na dhumna, lakini hakuwahi kumuuliza juu ya habari za wazee na ndugu zake, japokuwa kwenye maisha yake alipenda kudadisi na kupata habari, hatua iliyopelekea yeye kuwa mwandishi tangu akiwa shule ya msingi
“Mzee Karume alipendeza kukaa mtaani kwa kuwa mtu wa mikasa, siku zote jua lilipochomoza alipenda kupiga soga katika baraza la kahawa mbele ya nyumba yetu, miongoni mwa alikuwa anazungumzanao alikuwa baba yangu, mjomba wangu Suleiman Shebe ‘Madawa’, Rashid Mbarouk, Muhsin na Aboud Maalim, Abeid (muuza vifuu), Abaa aliyekuwa fundi wa baiskeli na mzee mmoja fundi mwashi, Mwinjuma aliyemchukua Ikulu alipokuwa Rais” -Salim
Aidha, anaendelea kusimulia kuwa miongoni mwa mambo yasiyobishaniwa kuhusu maisha ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ni kwamba alizaliwa mwaka 1905 na kupata elimu ya msingi katikati ya miaka ya 1910, ambapo baada ya masomo alikuwa baharia katika meli za mizigo na kila aliporudi safarini alimletea (yeye Salim) paketi za Peremende, Chokoleti na Biskuti
Kupitia makala ile aliyoichapisha kwenye gazeti la Mwananchi siku za nyuma, Salim ambaye sio tu mwandishi wa habari, lakini pia alikuwa mtu wa karibu na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume anaendelea kueleza kuwa baadaye (Sheikh Karume) alijiunga rasmi na chama cha mabaharia wa Uingereza kilichokuwa na makao yake makuu jijini Liverpool, ambapo kupitia hapo hakushangaa kumuona akishabikia klabu ya Liverpool katika wakati ambao idadi kubwa ya wazee wenzake wa mtaani walikuwa wakishabikia vilabu vingine kama vile Blackpool, Leeds, Everton, Westham United, na Sheffield United
Inaelezwa pia, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa mwanachama wa Yanga SC ya jijini Dar es Salaam na kupitia hilo inaelezwa kuwa ilikuwa ukifika ukumbini kwake ulikuwa unakutana na picha alizopiga na wazee wa Yanga SC katika miaka ya 1948 na kuendelea, ambapo iko wazi kuwa alipokuwa Rais alitoa fedha zake binafsi kusaidia ujenzi wa makao makuu ya Yanga SC yaliyopo eneo la Jangwani (Kariakoo) jijini Dar es Salaam akiwa sako kwa bako na mke wake mama Fatma Karume ambaye mpake leo hafichi mapenzi yake kwa klabu hiyo, na ni Mjumbe wa kudumu wa Baraza la Wadhimini wa Yanga SC
“Siku moja tulipokuwa uwanjani kuangalia mpira nilimuona akisherehekea goli maridadi lililoizamisha timu yake ya Kisimamajongoo, aliipenda klabu ya Liverpool kwa sababu alipokuwa baharia meli yake ilifika sana katika bandari hiyo ambayo mji wake una historia ndefu ya Waafrika kuishi hapo zaidi ya karne nne zilizopita, Mzee Karume aliiona Liverpool kama timu ya mabaharia wenzeke” -Salim
Inaelezwa kuwa, mapenzi yake kwenye sekta ya michezo ndio yaliyopelekea kuipatia Zanzibar uwanja wa Amani mara tu baada ya yeye kuingia madarakani kama Rais wa Zanzibar, na kwa wakati huo uwanja huo ndio uliotajwa kuwa bora zaidi Afrika Mashariki na Kati, ambapo alisisitiza amani katika michezo wakati wote na kusema hapana haja ya uhasama na labda ndio maana alifurahia hata timu aliyoipenda ilipofungwa bao safi
Watu waliomfahamu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume hawakushangazwa siku moja kati ya mwaka 1969 au 1970 alipokuwa jukwaa kuu akiangalia mpira kati ya Mwadui na Miembeni ya Zanzibar alipoamuru mchezo huo uvunjwe kabla ya muda kwa vile aliona Mwadui wanacheza rafu, ambapo alitoa amri ya kwamba Mwadui watolewe uwanjani na Jeshi la Polisi na wapelekwe moja kwa moja uwanja wa ndege na kuondoka Zanzibar, sambamba na kuipiga marufuku timu hiyo kufika Zanzibar, na inaelezwa Mwadui haikuwahi kukanyaga tena Visiwani Zanzibar enzi za uhai wake, ha ha ha huyo ndo Sheikh Abeid Amani Karume
Wafuatiliaji wa masuala ya michezo watakuwa wanakubaliana nami kuwa kila alipokuwa akizungumzia masuala ya soka na michezo kwa ujumla kwenye hotuba zake hakuacha kusisitiza kuwa ‘soka ni mchezo wa waungwana na ni watwana ndio wanaocheza rafu’
Kutokana na kutopenda watu kuumizana katika michezo Hayati Sheikh Abeid Amani Karume alipiga marufuku mchezo wa ngumi (ndondi) kufanyika Visiwani Zanzibar, na amri hiyo itakumbukwa kuwa imedumu kwa miaka mingi Visiwani humo kabla ya kuondolewa hivi karibuni Agosti mwaka 2023 baada ya Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuruhusu mchezo huo baada ya amri hiyo iliyodumu kwa takribani miaka 50
Tukirejea kwenye makala ya Salim, anasema siku moja akiwa na mwandishi mwenzake maarufu hapo zamani Mohamed Karim (baba wa mtangazaji Farouk Karim wa ITV) alimuuliza kwa nini hapendi ndondi, lakini jibu lake lilikuwa fupi tu ambalo ni la kukata na shoka ambapo alimjibu, “Eboo! We Shtobe (jina la utani la Salim alilolipata kufuatia kupenda sana kupigana bila ya sababu) unapigana na mwenzako ili iwe nini?, ukitaka kupigana pigana na tumbo lako, na sio na mwenzako”
Wakati timu ya Zanzibar ilipopiga kambi kwa michuano ya mwisho ya kombe la Gossage 1966 (sasa Chalenji) ilipofanyika Zanzibar, inaelezwa mzee Karume alionekana akiitembelea timu hiyo asubuhi na jioni, ambapo aliangalia hali ya malazi na chakula na kutazama mazoezi na hata kutoa maelekezo kwa wachezaji, kwani yeye binafsi (Sheikh Karume) alikuwa hodari wa kucheza dhumna, bao na karata, na kwamba walipokuwa wakirusha kishada hakupenda kile kilichokuwa na mkia kwa kuwa hali hiyo ilionyesha kukosekana ustadi katika kukitengeneza
Ukizungumza na watu wake wa karibu na wale waliokuwa mashuhuda wa matendo yake ya kimichezo enzi za uhai wake, wanasema mara nyingi Sheikh Abeid Amani Karume alifika kuangalia mpira bila ya taarifa ya mapema, kwani hata timu ndogo zilipocheza uwanja wa Mao Dzedung pia alihudhuria mara kadhaa, ambapo kuna wakati alikuwa akifika uwanjani na kukuta jukwaa kuu wamekaa watoto, alichokifanya ni kukaanao pamoja kama na yeye ni mtu wa kawaida, na walikuwa wanaangalia mchezo pamoja hadi mwisho.
TUANGALIE SASA KIFO CHAKE
Hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kipigwa risasi Aprili 7.1972, ambapo inaelezwa kuwa risasi nane zilitolewa mwilini kwake, pindi mwili wake ulipofikishwa kwenye Hospitali ya V. I. Lemin, mjini Unguja (Zanzibar) kwa uchunguzi, inadaiwa risasi hizo nane unaweza kusema ni sawa na idadi ya miaka minane ya utawala wake ulioanza 1964 hadi kifo chake.
TUKIO LA RAIS KUPIGWA RISASI LILIKUWAJE?
Sheikh Abeid Amani Karume na Makomredi wenzake wa Chama cha Afro-Shirazi -ASP (ambacho baadaye kilikuja kuunganishwa na TANU cha Tanganyika na kuunda CCM) alikuwa na mazoea ya kucheza karata, dama au dhumna kwenye ukumbi wa ofisi za makao makuu ya chama hicho Kisiwandui, kila jioni kama sehemu ya mapumziko
Siku hiyo ya tukio, inaelezwa Sheikh Karume alifika saa 11.00 jioni akiwa na walinzi wake, akaingia ndani nao wakabaki nje kulinda, ikafika zamu yake kucheza; akawa anacheza na Mzee Maalim Shaha Kombo ambaye alionekana kuelemewa na mchezo, ndipo Sheikh Karume akamuita Mzee Mtoro Rehani ajitayarishe baada ya Kombo, naye akaitikia kwa kuaga kwanza aende msalani kujisaidia, lakini sekunde chache baada ya hapo na kabla Mzee Mtoro Rehani hajarejea kutoka msalani, ghafla watu wawili wenye silaha walivamia chumba alimokuwa Sheikh Karume na wenzake na kumimina risasi wakimlenga Sheikh Karume
Kufumba na kufumbua Sheikh Karume akawa katika dimbwi la damu kimya, amepoteza uhai, hakuna mtu mwingine aliyeuawa mbali na kujeruhiwa tu, mmoja wao akiwa Katibu Mkuu wa ASP wakati huo Hayati Sheikh Thabit Kombo Jecha, risasi uaji (the fatal bullet) mbali ya risasi zote, iliyochukua uhai wa Sheikh Karume ilitoka kwenye bunduki ya Luteni Hamoud Mohammed Hamoud wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa uvamizi huu na aliyefyatua risasi ya kwanza wakati Sheikh Karume akicheza na wenzake, inasemekana Hamoud aliuawa papo hapo na mlinzi wa Sheikh Karume
Wauaji wengine waliofuatana na Hamoud katika uvamizi huo ni Kapteni Ahmada Mohamed, Koplo mmoja wa Jeshi ambaye jina lake halijafahamika hadi leo, na raia mmoja aliyetambulika kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao inaelezwa wote hao waliuawa kwenye mapambano ya silaha nje ya eneo la tukio, dakika chache baada ya mauaji kutokea alifika Kanali Ali Mahfoudhi na askari mwingine, Kapteni Makame Hamis wakauchukua mwili wa Sheikh Karume na kuukimbiza Hospitali.
Kanali Mahfoudhi alikua ni mmoja wa vijana wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu, chama kilichoungana na ASP baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12.1964 na kuunda serikali ya mseto Visiwani humo, ni kati ya vijana waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi, na ni mmoja wa wapiganaji walioendesha mapambano ya kisayansi usiku wa Mapinduzi na kukamata uwanja wa ndege mchana Aprili, 1972
Kama hiyo haitoshi, huyu pia ni mmoja wa wanaharakati wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ambao hawakutakiwa Zanzibar wakati wa utawala wa Sheikh Karume, kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26. 1964, Sheikh Karume alishinikiza kwa Nyerere wapewe kazi Tanzania Bara aweze ‘kupumua’ ambapo Mahfoudhi alipewa cheo cha Mkurugenzi wa Operesheni katika JWTZ
Wengine ambao hawakutakiwa ni pamoja na Babu mwenyewe aliyepewa Uwaziri wa Mipango ya Uchumi kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasimu mwingine wa Sheikh Karume, Othman Sharrif, ambaye alifanywa Afisa Mifugo wa Mkoa, Mtwara, na Balozi Salim Ahmed Salim wakati huo Balozi wa Zanzibar nchini Misri ikaridhiwa aendelee kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo
Kuna dhana mbili kinzani kuhusu jinsi Sheikh Karume alivyouawa na hatima ya wauaji,.dhana moja inadai kwamba, watu wanne walivamia mahali alipokuwa Sheikh Karume na wenzake wakamimina risasi mara nne au mara tano hivi, risasi ya kifo ikampata Sheikh Karume shingoni akafa, huku zingine zikiendelea kumiminwa kulenga meza walipokuwa, ambapo inadaiwa kuwa Hamoud aliuawa kwenye eneo la tukio, ambapo wawili waliuawa baadaye na vyombo vya usalama (kwa mapambano) na mmoja alijiua
Dhana ya pili inadai kwamba Hamoud alikufa kwenye eneo la tukio katika mazingira ya kutatanisha, ama kwa kujipiga risasi kuepuka kukamatwa hai na kuteswa baada ya kuona asingeweza kutoroka, au alijeruhiwa vibaya na walinzi wa Karume, kisha Ahmada akampiga risasi na kumuua kumuepusha kuteswa na kutoa siri kama angekamatwa hai, kisha (Ahmada) akaweza kutoroka kwenye eneo la tukio, kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa juu ya kuhusika au kutohusika kwao na mauaji, wengi wakiwa viongozi na wanachama wa zamani wa Umma Party, chama cha Babu na wanachama mashuhuri wa ASP wenye siasa za mrengo wa Kikomunist.
Ni machache kati ya mengi kumuhusu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya mpendwa wetu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mahala pema Peponi, Amina.