Latest Posts

SHERIA ZINAZOTUNGWA NA BUNGE ZADAIWA KUWADIDIMIZA WAFANYAKAZI

Theophilida Felician, Kagera.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Kagera na Rais mstaafu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Gration Mukoba amesema sheria  zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndizo zinazopelekea mambo mengi kutofanyika kwa weledi na kwa ufanisi nchini.

Mukoba ameyabainisha hayo akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kitongoji cha Buhanga kata ya Buganguzi, Muleba Kaskazini ambapo amefafanua kwamba kuna baadhi ya sheria zinazotungwa na bunge hugeuka kuwa kandamizi kwa wafanyakazi katika masuala kadhaa ikiwamo mishahara na kiinua mgongo. 

“Wabunge wanavyokuwa wanapitisha sheria za ajabu ajabu na sheria mbovu wenyewe mbona hawajitungii? Wabunge wanapata kiinua mgongo baada ya miaka tano, kiinua mgongo chao hakikatwi hata senti moja, walimu na wafanyakazi wengine wanapata kiinua mgongo chao baada ya miaka 30, 33, hadi 40” Amefafanua Mukoba.

Mbali na hayo amegusia changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya elimu hususani uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule hali inayopelekea walimu kufundisha wanafunzi wengi madarasani ikilinganishwa na uwiano wao.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuichagua CHADEMA ili kuyafanyia marekebisho ipasavyo yale yote ambayo yamekumbatiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo amesema yamesababisha changamoto kwa umma. 

Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera Danieli Damian amekemea vitisho alivyodai kufanyiwa wanachama wa chama hicho kutoka kwa wanachama wa CCM huku akiwasisitiza wananchi kuhakikisha wanajiandikisha ili kuweza kuwachagua viongozi bora ambao alidai watatoka CHADEMA.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la  Bukoba Mjini Chief Karumuna akiambatana na viongozi wenzake amezungumzia suala la serikali kutokuchukua hatua kwa watu wanaohusika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma licha ya ripoti ya CAG kuubaini. 

Chief pia amekemea vikali tukio la kupotea  kwa watu wawili miaka miwili iliyopita katika kata ya Kishanda huku akiapa  kupambana usiku na mchana kuhakikisha watu hao wanapatikana pasina kuzingatia kama wangali hai ama wafu.

“Tuna mtu anaitwa Mzee Msukuma pale Kishanda ana watoto  Amoni na Singi mnawafahamu, tuna miaka miwili hawa watu hatunao,”Amesema Chief Karumuna. 

Hata hivyo ametoa wito kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya Muleba  na viongozi wengine wa serikali kushughulikia jambo hilo ili watu hao waweze kurejeshwa katika familia zao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!