Latest Posts

SHILINGI BILIONI 184 KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI TARIME NA RORYA

Na Fredrizzo Samson, Tarime.

Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) ipo katika mkakati wa kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi bilioni mia moja na themanini na nne utakaomaliza changamoto za maji, ambao tayari serikali imeulipia billioni ishirini kwa mkandarasi na kuanzishwa utekelezaji wake.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Nickas Mugisha alipokuwa akikabidhi vifaa vya ujenzi wa vituo vya kuchotea maji katika kata ya Sabasaba vitavyokwenda kujenga ‘DP’ za maji zitakazohudumia wakazi wa mitaa mitatu ya kata hiyo ambayo ni mtaa wa Chomete, Nyangai na Kimusi.

“Huu ni mradi wa maji wa muda mfupi ambapo hapa kuna tenki lenye ukubwa wa lita laki tatu (300,000) na kuna pampu mbili ambazo zinaweza kuzalisha lita elfu ishirini na mbili (22,000) kwa saa moja, Tarime kumekuwa na uhaba wa vyanzo vya maji kulinganisha na uhitaji wa watu kwa hiyo miradi hii tunayofanya ni kuwapatia watu maji kwa muda mfupi lakini upo mradi mkubwa wenye gharama ya bilioni mia moja themanini na nne (184,000,000) ambao serikali tayari imeishalipa bilioni ishirini na mkandarasi anaendelea na kazi, huo ndio mradi mkubwa ambao ukikamilika utapeleka maji sehemu zote za wilaya ya Tarime na Rorya”, amesema Nickas Mugisha, Mkurugenzi MUWASA.

Wakipokea vifaa hivyo kwa niaba ya wananchi wenyeviti wa mitaa hiyo mitatu wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa kuendelea kuwaletea miradi katika kata yao ya Sabasaba.

“Tunaamini sasa tutakwenda kuepukana na magonjwa ya tumbo ya mara kwa mara yatokanayo na maji ambayo si salama na safi hivyo ni jukumu langu mimi mwenyekiti kuhamasisha wananchi wangu kujivutia maji kwenye maeneo yao sambamba na kulinda vyanzo hivyo ili vitunufaishe kwa miaka mingi”, amesema James Nyangai ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kimusi, huku John Peter ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Chomete amesema,

“Katika mtaa wa Chomete vilipatikana vyanzo viwili vya visima ambapo kimoja kinatoa Lita 15000 kwa saa na cha pili kinatoa lita 7000 kwa saa ambapo kwa wastani wa saa moja kwenye visima vyote viwili vinatoa lita 22,000 kwa saa moja na maji hayo yamesambazwa katika kata tatu ya Sabasaba, Nkende na Nyamisangura”.

Jambo TV imefanya mazungumzo na mwananchi Abgael Zabron (47) kwa niaba ya wengine waliokusanyika eneo hilo ambapo ameeleza furaha yake na kero ambayo bado ni changamoto.

“Bado ipo changamoto kubwa kwa upande huu wa maji kukatika mara kwa mara na kutoka mara mbili tu kwa wiki suala hilo bado linatuumiza sana wananchi wa maeneo haya tunaomba hilo nalo likomeshwe”, amesema Zabron, mkazi wa Mtaa wa Chomete.

Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi kata ya Sabasaba ambaye tangu mwanzo alikuwepo kusimamia makabidhiano hayo ameiambia Jambo TV ya kuwa licha ya kupata mradi huo wa maji kata ya Sabasaba lakini kumekuwa na changamoto ya usambazaji wa mabomba kwenye mitaa.

“Ninamshukuru mkurugenzi kwa kutuletea vifaa hivi vitakavyowezesha kujenga ‘DP’ za kuchotea maji kwenye mitaa mitatu na ametueleza atazidi kuleta vifaa hivyo na kwenye mitaa mingine, Rai yangu kwa viongozi wa mitaa vifaa hivi visiende kukaa ofisini bali wakasimamie ufungwaji wake haraka ili wananchi wetu waanze kufurahia huduma”, ameeleza Charles.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!