Latest Posts

SHILINGI BILIONI 37 ZATUMIKA KUKARABATI NA KUPANUA KIWANJA CHA NDEGE CHA SONGEA

Serikali imetangaza kuwa takriban shilingi bilioni 37 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Songea, hatua ambayo inatarajiwa kuchochea ongezeko la safari za ndege na kukidhi mahitaji ya wasafiri wa anga Mkoani Ruvuma.
 
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kukagua maboresho katika kiwanja hicho.
 
Waziri amesema kuwa maboresho hayo ni muhimu kwa kuongeza idadi ya safari za ndege, huku akibainisha kuwa shirika la ndege la Air Tanzania tayari limeanza safari mara tatu kwa wiki na kuna mpango wa kuongeza safari hadi mara tano kwa wiki, na baadaye kufanya safari za kila siku,.
Ameeleza pia kuwa kwa sasa wananchi wataendelea kutumia jengo dogo la abiria, huku serikali ikiendelea na mchakato wa kujenga jengo jipya la kisasa ambalo litaendana na hadhi ya kiwanja hicho na kutoa huduma bora kwa abiria.
 
“Tunafanya kazi ya kuboresha jengo la muda kwa sasa, lakini mpango ni kujenga jengo jipya la kisasa ambalo litatoa huduma bora zaidi kwa wananchi wetu,” ameongeza Mbarawa.
Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameshukuru serikali kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya uchukuzi na utekelezaji wa miradi chini ya Wizara ya Uchukuzi.
 
“Nakushukuru kwa jinsi unavyoupa mkoa wetu kipaumbele, hasa katika sekta zinazohusiana na wizara yako. Hii ni hatua muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa mkoa wetu,” amesema Kanali Ahmed.
 
Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songea, Mhandisi Danstan Komba, amebainisha kuwa maboresho ya miundombinu yameongeza idadi ya abiria kutoka 3,000 kwa mwaka kabla ya 2021, hadi kufikia 19,300 kwa mwaka.
 
“Kabla ya mwaka 2021, tulihudumia abiria takriban 3,000 kwa mwaka, lakini tangu Air Tanzania ilipoanza tena safari zake mnamo Novemba 2021, sasa tuna uwezo wa kuhudumia abiria 19,300 kwa mwaka. Haya ni mafanikio makubwa kwa mkoa wetu,” amesema Mhandisi Komba.
 
Ameelezea pia kuwa maboresho hayo yamehusisha upanuzi wa njia ya kutua na kurukia ndege, ambayo sasa imeongezeka urefu kutoka mita 1,600 hadi mita 1,860, hivyo kuboresha usalama wa ndege zinazotua na kuruka.
 
Pia amesema kuwa serikali imeimarisha eneo la usalama kwa kusimika taa za kuongozea ndege, kuwezesha safari za usiku na wakati wa hali mbaya ya hewa kama ukungu.
 
Mengine yaliyoboreshwa ni pamoja na kituo cha kupokea nishati, ikiwa ni pamoja na maji na umeme, kupitia mfumo wa umeme wa kilowatt 33, pamoja na barabara ya lami yenye viwango vya kimataifa inayokidhi mahitaji ya uendeshaji wa ndege.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!