Zaidi ya Shilingi bilioni 32 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na ukarabati wa miundombinu kwenye idara ya elimu sekondari katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza siku ya Jumamosi wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 4.6 zimetumika kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Kitunda, itakayokuwa ya kisasa na ya ghorofa.
Mpogolo amesema ujenzi wa shule hiyo umetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba sasa halmashauri hiyo inaonyesha nguvu ya ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo.
“Shule hii itakuwa na ghorofa nne, madarasa 16, maktaba ya kisasa, maabara nne na ofisi 12. Napenda kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kuona umuhimu wa ujenzi wa shule za kisasa kama hizi,” alisema Mpogolo.
Amemtaka Mkurugenzi wa Jiji kuhakikisha kuwa mkandarasi anakamilisha ujenzi huo kabla ya Februari 2026, ili iweze kuwapokea wanafunzi kutoka Kata ya Kitunda, Kivule, Ukonga, Kipawa na Kipunguni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na utaondoa changamoto ya mrundikano wa wanafunzi darasani.
“Kwa sasa tupo katika hatua ya ujenzi wa ghorofa la kwanza, lakini mradi huu utasaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia,” amesema Mabelya.