Walimu, wazazi, walezi na Watanzania kwa ujumla wameaswa kuendeleza vipaji vya wanafunzi walioko shuleni na wanaohitimu, kwa lengo la kuhakikisha vipaji hivyo vinawanufaisha katika maisha yao ya kitaaluma na kijamii.
Rai hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, wakati wa mahafali ya wanafunzi wa kidato cha sita wa Sekondari ya Green Acres, yaliyofanyika Jumamosi, Aprili 5, 2025 mkoani Dar es Salaam.

“Green Acres mmefanikiwa sana kitaaluma. Naomba mviendeleze vipaji vya hawa vijana. Wanafunzi hawa mmewalea miaka miwili, mnajua uwezo wao. Kuna mwanafunzi anaweza kulazimishwa kuwa mhandisi lakini kipaji chake kiko kwenye sanaa au michezo,” amesema Meya Kumbilamoto.
Akijibu ombi la shule kuhusu changamoto ya barabara inayounganisha shule hiyo na barabara kuu ambayo huwatatiza wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo hasa kipindi cha masika, Meya Kumbilamoto ameahidi kulifikisha kwa mamlaka husika ili lizingatiwe kwenye Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambao huhusisha barabara zinazoingia mitaani.

Aidha, amesifu uwekezaji wa Green Acres katika sekta ya elimu, ikiwemo kuwa na zahanati shuleni, akisema ni mfano bora unaopaswa kuigwa na shule nyingine, na kwamba yeye mwenyewe atakua balozi wa shule hiyo kwa kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao hapo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shule za Green Acres, Jacklyne Siima Rushaigo, amesema shule hiyo inaadhimisha miaka 25 ya mafanikio makubwa katika elimu. Maadhimisho hayo yatahusisha ibada za shukrani, siku ya wazazi, ziara za kijamii na Salasala Marathon ambayo imelenga kuunganisha jamii na kuchangia afya.
“Tunasherehekea mafanikio haya tukiwa na shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya elimu. Sera jumuishi zimewezesha shule binafsi kama yetu kusimama imara,” amesema Rushaigo.

Amewahimiza wahitimu kuendelea kudumisha maadili, nidhamu na hofu ya Mungu ili kufanikisha ndoto zao.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Jonathan Kasabila, amesema shule imeendelea kung’ara kitaaluma kupitia matokeo mazuri ya mitihani ya kitaifa kwa ngazi zote. Pia ameeleza jinsi shule hiyo ilivyojipambanua kwa kuwa na mazingira bora ya kufundishia, makazi ya walimu, na huduma za afya shuleni.
Mwalimu Kasabila pia amekanusha dhana potofu kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa shule binafsi, akisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitoa mikopo bila ubaguzi kwa wanafunzi wote wanaostahili.

“Hili ni jambo la msingi ambalo tunapaswa kulielewa – hakuna mwanafunzi anayepoteza fursa ya mkopo kwa sababu tu ametoka shule binafsi,” amesisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Queen Joel Ilanda, amesema wanafunzi wamefanya kazi kwa bidii hadi kufikia hatua ya kuhitimu, huku akitoa wito kwa shule kuboresha eneo la upatikanaji wa vifaa na huduma za kidijitali, kwa ajili ya kuongeza tija katika elimu. Zaidi ya haya yote, ameahidi darasa lao kufanya vizuri katika mitihani ya taifa na kuzidi kupamba na kuipa sifa shule yao.
