Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya ziara ya kikazi katika maeneo ya Bumbuli, Lushoto, Mkomazi, na Korogwe, ambapo alikagua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi. Katika ziara hiyo, amesisitiza mshikamano kati ya serikali na wananchi katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania. Aidha, amewataka viongozi wa maeneo husika kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.
Akiwa Wilayani Korogwe, Rais Dkt. Samia ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Bwawa la Mkomazi pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji za Mkomazi na Chekechea. Mradi wa Mkomazi, wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 18, unatarajiwa kuhudumia vijiji 28 katika kata saba za Wilaya ya Korogwe na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025.
Katika Wilaya ya Bumbuli, Rais alizindua jengo la Halmashauri ya Wilaya, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya mkoa wa Tanga. Kuanzia mwaka 2021 hadi mwanzoni mwa mwaka huu, takribani shilingi trilioni 3.1 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku sekta ya afya pekee ikipokea shilingi bilioni 65.6 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa mkoa huo.