Inafahamika kwamba kila ifikapo Oktoba 01 ya kila mwaka Dunia huadhimisha ‘Siku ya Wazee’ naaam ndivyo ilivyokuwa Tanzania kama nchi zingine zilizomo Duniani nayo imeshiriki siku hiyo kikamilifu, ambapo tumeshuhudia wazee kupitia taasisi na vikundi mbalimbali wakikutana na kujadili ajenda zinazowahusu kwa maslahi yao wazee wa sasa na hata wazee watarajiwa, shughuli hiyo Kitaifa imefanyika mkoani Tabora ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa mkoa wa Tabora Paulo Chacha
Siku moja kabla ya hiyo yaani Septemba 30.2024 kupitia kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii za chama kikuu cha kikuu cha upinzani nchini yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tumeshuhudia ikichapishwa taarifa inayosema, “Baraza la Wazee CHADEMA (BAZECHA) kupitia Mwenyekiti Taifa Mheshimiwa Hashim Juma Issa litazungumza na Watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari kesho, Oktoba Mosi 2024, saa tano asubuhi, makao makuu ya Mabaraza, Ufipa Kinondoni, waandishi wote mnakaribishwa”
Kwa wanahabari ilikuwa ni taarifa inayowahusu kama sehemu ya majukumu yao na wajibu wao kwenye jamii kufika mtaa wa Ufipa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam ilipokuwa makao makuu ya zamani ya chama hicho ili kuweza kuuhabarisha umma juu ya kinachoendelea kwenye mkutano huo wa Baraza la Wazee wa CHADEMA (BAZECHA)
Siku ikafika, na muda ukawadia kama ilivyotarajiwa Mzee Hashim Juma Issa na wazee wenzake wa chama hicho kama sio wafuasi wa CHADEMA walioambatana na Mjumbe huyo ya Kamati Kuu wakajitokeza mbele ya wanahabari ambapo tumeshuhudia hoja nyingi, mijadala na maoni ya wazee hao yakiwasilishwa kwa Watanzania kupitia wanahabari huku wafuasi waliojitokeza kumsindikiza mara kadhaa wakishuhudiwa wakisindikiza hotuba yake kwa kushangilia na kupiga makofi kama ishara ya kumuunga mkono kila anachokiwasilisha
Mzee Hashim Juma Issa katika mazungumzo yake pamoja na mambo mengine alionesha kumpongeza Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe pamoja na familia yake kwa kushiriki katika mstari wa mbele kukemea vitendo vya utekaji, unyonyaji na mauaji, sambamba kuwa kutoka hadharani na familia yake kwenye siku ya maandamano, katika hali isiyitarajiwa ghafla mada ikabadilika ‘hewani’, kwa lugha rahisi unaweza kusema ni kama gari lilikuwa linashuka kwenye mteremko na kufika chini ambapo ni mwanzo wa mlima mwingine hivyo dereva hulazimika kubadili gia pamoja na kukanyaga kiongeza mwendo (accelerator) ili gari iweze kupanda mlima huo
Ndivyo ilivyokuwa siku ile kwa Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa Mzee Hashim Juma Issa, kwa namna alivyobadili mada kutoka kwa Mbowe hadi kuelekea kutangaza hoja ambazo dhahiri shairi ni za udini, na Uzanzibar, Mzee huyo alinukuliwa akisema, “saluti kwako Mheshimiwa Mbowe, sasa hapo ndiyo unajua kwamba Watanzania wote kilio chao wanaililia CHADEMA ushanifahamu eeh…, CHADEMA ndio chama peke yake kinaweza kuwakomboa maskini, wanyonge wasiokuwa na sauti na hata kuwasemea ni CHADEMA tu
Kutoka hapo, ghafla! Mzee Hashim Juma Issa akakanyaga mafuta akaanza kusema, “jambo la kwanza mama Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan) shirikiana na Hussein Mwinyi (Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi), wewe ni muislamu, Hussein Mwinyi ni muislamu, Wazanzibari sote ni waislamu asilimia 98%, jambo la kwanza ni kuwapatia ajira vijana wa Kizanzibari, Wazanzibari wapo watu karibu milioni mbili ambapo zaidi ya milioni ni vijana wa Kizanzibari ambao hawana ajira”
Naomba nikurudishe mtaani kidogo hasa kule kwetu uswahilini kabisa, kuna kale kamsemo kanasema “maa’ke hapo kwanza n’cheke”, unaweza kujiuliza kwanini nimerudi kwetu uswahilini?, ngoja tuendelee utanielewa tu, watu waliohudhuria kwenye shughuli ile wengi wao kama sio wote ni wazee na wanachama kama sio wafuasi wa CHADEMA ambapo naamini wengi wao ni wakazi wa Dar es Salaam lakini ukichimbua asili ya kila mmoja utagundua wanatoka kila kona ya Tanzania hapa namaanisha inaweza kuwa Kusini, Kaskazini, Magharibi, Mashariki, Tanzania Bara au Visiwani, lakini pia watu hao naamini wanatoka kwenye makabila tofauti na hata dini na imani tofauti, ni imani yangu kuwa pale kulikuwa na wakristo, waislamu, wasio na dini na hata wanaoamini katika mizimu ya mababu zetu, lakini pale walikutanishwa na CHADEMA yao na Tanzania yetu kumbuka hiyo ni imani na mtazamo wangu,
Kwenye kanuni za uneni kwa umma (public speaking) moja ya kanuni inasema hakikisha unaijuwa hadhira unayozungumza nayo, Mzee Hashim Juma Issa tumeshuhudia akizungumza katika majukwaa mengi Tanzania Bara na Visiwani je, ni kwamba hakujuwa anazungumza na Watanzania na sio Wazanzibari?, kwanza vijana wa leo ni wazee wa kesho, vijana aliokuwa anawaombea ajira hapo ni wa Zanzibar maana yake alikuwa anataka kuandaa wazee bora wa kesho kwa Zanzibar na sio Tanzania, pili ilikuwaje akahama kwenye ajenda ya kumsifia Mbowe na chama chake na ghafla akaangukia kwa Rais Samia, Mwinyi na Wazanzibari?, sitaki kuamini na katu sitaweza kuamini kuwa ile imekuja kwa bahati mbaya, leo wapo vijana wa Zanzibar wanasoma Tanzania Bara na wanapata ajira Tanzania Bara kama ilivyokuwa pia vijana wa Tanzania Bara wanaosoma Zanzibar na pengine kupata ajira Zanzibar iwe ni ajira rasmi au isiyo rasmi, sasa Mzee Hashim Juma Issa amewahi kushuhudia vijana wa Tanzania Bara pekee kuzungumzia matatizo ya ajira yao pekee na sio Tanzania nzima
Katika sehemu ya hotuba yake amenikuliwa akisema kuwa, “sasa hivi Zanzibar jiunganisheni na OIC (Organization of the Islamic Cooperation) Nyerere (anamaanisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) hayupo, tupo peke yetu sasa hivi (watu wakacheka na kupiga makofi), tupo wenyewe sasa hivi, tupo waislamu watupu (anamaanisha serikali zote mbili za Tanzania yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinazongozwa na viongozi wakuu waislamu), hapa ndiyo pa kuchomoka, hapa ndiyo pa kujiunga na OIC, asije akaja mwingine huko mbele ya safari (anamaanisha anaweza kuja kiongozi mkiristo) ikawa balaa tena (Mzee Issa akaanza kutaja baadhi ya viongozi na watu wenye ushawishi walio katika dini ya kiislamu) Kikwete pale, Kassim Majaliwa pale, Hajjat Samia pale, Waziri wa mambo ya nje Mahmoud Thabit Kombo muislam, Waziri wa mambo ya ndani Hamad Masauni muislam, Rais wa Zanzibar muislam hapo ndiyo pa kujiunga na OIC msichelewe kabla hajaja Rais mkristo”
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, “kutafuta uongozi kwa kutumia ukabila au kwa kutumia dini unagawa watu.., mambo haya ya kuchochea chuki ama za ukabila ama za dini yakianza na tukayapa nafasi mtashangaa mnaanza kuchinjana na hakuna wa kumtetea mwenzake”
Najiuliza, Mzee Hashim Juma Issa alitumwa na CHADEMA?, au alitumwa na vijana wa Kizanzibari?, au alitumwa na viongozi wa serikali walioko madarakani ambao ni waislamu?, kama alitumwa nataka kujuwa huyo aliyetuma ni nani na ana maana gani?, na kama hajatumwa kwa nini Mzee Hashim Juma Issa atumie aseme maneno yale makali tena kwa kujiamini kabisa?, nani yuko nyuma ya Mzee huyu?, na kwa nini ajenda hii iwasilishwe kupitia jukwaa la CHADEMA?, maswali ni mengi sana kwenye jambo hili
Oktoba 02.2024, CHADEMA kupitia Mkurugenzi wake wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje John Mrema wametoa taarifa ya kukataa na kukanusha vikali kauli zozote zenye viashiria ya udini ambazo zimetolewa kwenye mkutano huo, “tunajitenga na kauli zote zilizotolewa zenye viashiria vya udini kwani huo sio msimamo wa chama na zinapaswa kupingwa na kila Mtanzania bila kujali dini, kabila au anapotoka”
Kwanza, nianze kwa kuwapongeza CHADEMA kwa taarifa ya kujitenga na matamko hayo, lakini niwe muwazi hapa nimesoma kwa makini sana taarifa ya CHADEMA kiukweli kwangu imeniongezea maswali kuliko majibu niliyotarajia, CHADEMA wanasema wanajitenga na kauli za Mwenyekiti wa BAZECHA Mzee Hashim Juma Issa juu ya udini, maana yake wanamuunga mkono kwenye mambo mengine aliyozungumza pale sio?, kama hawamuungi mkono kwenye hili maana yake hawamuungi mkono kwenye hotuba yake yote, sasa tutafakari wote hotuba ile aliandika nani?, kama walimuandikia wasaidizi wake maana yake chama kilijulishwa nini kinaenda kuongelewa, pia kama hakuandaa hotuba bali walikuwa na ajenda maalum walizojiandaa kuwasilisha kwa jamii ikiwemo hiyo ya Uzanzibari na Udini, kama yote hayo hayakuwepo hiya inajenga ukakasi kwamba chama kinawezaje kuruhusu mtu mmoja au kikundi cha watu fulani hata kama wana nafasi fulani kwenye chama hicho kutumia jukwaa la chama bila kuwa na ajenda stahiki?
Tusisahau kwamba huyu Mzee Hashim Juma Issa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA wa muda mrefu sana, sasa kama hawaungi mkono kauli zake kwa nini waliokuwa pale walikuwa wanapiga makofi?, waliokuwa wanapiga makofi ni kina nani? je, haya tuseme mamia ya wafuasi wote waliokuwa eneo lile la mkutano walikuwa wanamuunga mkono kwenye kila hoja mzungumzaji ndio maana walikuwa wanasindikiza hotuba kwa shangwe na makofi, lakini kutokana na tukio hilo kurushwa mubashara kupitia platform mbalimbali kwamba hapakuwa na viongozi wa chama hicho waliofuatilia kilichokuwa kinaendelea ili waweze kuipinga hiyo kauli haraka tena ndani ya muda mchache tangu kutolewa kwake
Imechukua karibu saa 24 ndipo taarifa ya CHADEMA ikatoka je, nafahamu kuwa imeelezwa hatua zinaendelea kuchukuliwa ndani, lakini kama tumeweza kujitenga na kauli zake kwa haraka tumeshindwaje kusema hatua za haraka tunazochukua au tulizochukua?, nasema hivyo kwa sababu najuwa kuwa taarifa iliyotolewa na CHADEMA si ya John Mrema bali ya chama so kabla ya kutoka kwa umma imeamuliwa na watu kadhaa, sasa hao waliofanya maamuzi hawakuona umuhimu wa hili au ndio ule usemi wa “mtu mzima hakosei bali anateleza”
Imani yangu inaniambia kwamba tamko la CHADEMA halijatoka kwa sababu chama hicho kimechukia la hasha, bali limekuja kufuatia ‘presha’ kubwa iliyokuwa inaendelea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo kwa kiasi kikubwa ‘mawe’ yalikuwa yanaelekezwa kwa kiongozi wao (Mzee Hashim Juma Issa) na chama kwa ujumla wake
Kama tunataka kuchukua hatua, je tunamchukulia hatua Mzee Hashim Juma Issa pekee au?, maana sina hakika kama tunawajuwa wale wafuasi waliopiga makofi pale kwenye mkutano, tukimchukulia hatua mtu mmoja basi tujuwe ndani yake kuna ‘virusi’ vingi vimezaliana
Katika mjadala wa jambo hilo nimeona hoja iliyoandikwa na Godbless Lema ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, ambapo anasema,
“Hii ni kauli mbaya sana, nafikiri kuna tatizo kubwa sana, nasikitika kuwa imetolewa na kiongozi kutoka katika chama changu, nashindwa kupuuza maneno haya kwa namna yoyote ile, maneno haya yanajengwa na mkakati wa siri ambao wengi tunaweza kuwa tunaiona lakini tunaogopa kuchukua hatua, siasa zenye misingi ya udini sio za bahati mbaya katika nchi hii, kauli chafu kabisa hii wala sio ya bahati mbaya, siri zikiwa nyingi moyoni huwa zinatoka zenyewe”
Sasa kwa kauli ya Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu anasema hii sio kauli ya bahati mbaya, nadhani hapa anaungana nami lakini kama sio kauli ya bahati mbaya, nani aliyepanga na kuratibu au anayeratibu dhambi hii kwa nchi yetu?, je huyo mtu au watu wako ndani ya CHADEMA au nje ya CHADEMA?, kama hawako ndani ya CHADEMA kwa nini jukwaa la CHADEMA litumike?
Lakini Lema anasema siri zikiwa nyingi huwa zinavuja, inamaana kumbe huenda Mzee Hashim Juma Issa ana ajenda za siri?, hizo ajenda anapanga na nani?, na huyo mtu au watu wako ndani ya CHADEMA au la?, lakini anaenda mbali na kusema wengi huwa tunaiona ila tunaogopa kuchukua hatua, kumbe huu mpango huenda Lema na baadhi ya watu ndani ya CHADEMA wanaujuwa?, kama hivyo wanaogopa kuchukua hatua kwa nani?, na kwa nini waogope?, kama mapenzi kwa chama na Taifa kwa nini tusichukue hatua?, huyo anayeogopwa ni nani?, kwa hiyo tunaogopa sasa ili mambo yaharibike zaidi huko mbele?, narudia tena maswali ni mengi mno kwenye jambo hili, kila anayechangia kwangu anaibua maswali mapya kabisa,
Ningeweza kuchukua zaidi ya saa 24 ‘kutapika’ maneno yangu kwenye jambo hili, lakini naona kila nikiandika najikuta naandika maswali zaidi kuliko majawabu jambo ambalo si lengo langu,
Makala hii ni kwa rafiki zangu wa CHADEMA na wafuasi wake, hawapaswi kuliangalia jambo hili kwa kawaida tu, hawapaswi kuliangalia jambo hili kwa jicho la kwamba Mzee Hashim Juma Issa katumwa na wapinzani wa CHADEMA, wanapaswa kuliangalia jambo hili kwa jicho la tatu, na sisi wapenzi watazamaji tunawamulika sana kwenye hili, tunajuwa mengi yanayoendelea hili ni mfano na moja wapo tu.
NB: makala hii imeandaliwa na Raidhani Mohamed na Fadhili Kirundwa