Latest Posts

SIKU 20 ZA MOTO KWA BONI YAI GEREZANI, NA MASHARTI MATATU YA DHAMANA MAHAKAMANI

Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Oktoba 07.2024 imempatia dhamana Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani Boniface Jacob (Boni Yai) aliyekuwa anashikiliwa kwenye gereza la Segerea tangu alivyokamatwa na Jeshi la Polisi kwa mara ya kwanza Septemba 18.2024 Golden Fork, kabla ya kufikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam

Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ametoa maamuzi hayo madogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili mshtakiwa huyo, ambapo maamuzi hayo yanakuja kufuatia pingamizi lililokuwa limeletwa na mleta maombi ambayo ni Jamhuri/ serikali iliyokuwa imeiomba Mahakama kutompatia dhamana Boniface Jacob (Boni Yai) kutokana na madai kwamba usalama wake utakuwa shakani akiwa uraiani

Awali kabla ya kusomwa kwa maamuzi hayo, Jamhuri/ serikali kupitia kwa Wakili wa serikali mwandamizi Job Mrema aliiomba Mahakama kuwasilisha maombi mapya Mahakamani hapo, jambo ambalo lilipingwa vikali na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Peter Kibatala, ambapo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Mahakama ilitupilia mbali maombi hayo badala yake ikajielekeza kwenye kusoma maamuzi yaliyokusudiwa

Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam alianza kwa kurejea kiapo cha RCO wa Kinondoni SSP David Msangi ambaye katika kiapo hicho ameeleza kuwa amepata taarifa za  kiiterejensia kuwa usalama wa mshtakiwa uko shakani hivyo kwa kunusuru uhai wake ni vyema akaendelea kuwa gerezani wakati shauri lake likiendelea

Sambamba na hilo kupitia kiapo hicho SSP Msangi alieleza kuwa mtuhumiwa mwenyewe Boniface Jacob (Boni Yai) alitoa maelezo hayo alipokuwa akihojiwa kwenye kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam ambapo inadaiwa kuwa aliwaeleza Polisi waliokuwa wanamuhoji kuwa kutokana na ‘uwongo’ anaouandika mitandaoni hivyo usalama wake uko hatarini kwa kuwa anahofia kutekwa na kuuawa

Inaelezwa kuwa upande wa utetezi katika kupinga hoja hiyo uliieleza Mahakama kuwa madai hayo hayana msingi kwa kuwa si kweli kwamba mtuhumiwa amedai kuwa usalama wake uko shakani, hivyo kuiomba Mahakama kutokubaliana na hoja hizo

Akifafanua hoja hizo baada ya kuzichuja Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu amesema kwa mara ya kwanza Mahakama ilijiuliza endapo kiapo cha waombaji na hoja zilizotolewa na pande zote mbili (2) zinaweza kuishawishi Mahakama kutompatia au kumpatia dhamana mshtakiwa,  huku Mahakama hiyo ikitambua kwamba mshtakiwa kupatiwa dhamana ni haki yake ya Kikatiba lakini pia usalama pia ni haki ya Kikatiba

Akiwa Mahakamani hapo Hakimu Kiswaga amerejea mashauri kadhaa yanayoshabihiana na hilo yaliyowahi kupokelewa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Juu ya Kenya na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo baadaye Hakimu alifafanua kuwa kosa aliloshtakiwanalo ni mtuhumiwa linadhaminika labda kuwe na sababu za msingi ambazo Mahakama itashawishika kuzuia dhamana hiyo

Akirejea kwenye hoja iliyokuwa mezani, Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu amesema sababu zilizowasilishwa na Jamhuri/ serikali hazijafafanuliwa kinagaubaga iwapo mshtakiwa alitoa maelezo ya kwamba usalama wake uko shakani mbele ya Jeshi la Polisi yeye mwenyewe, na kwamba Mahakama ilitarajia pengine waleta maombi wangewasilisha  uthibitisho wa hoja hiyo jambo ambalo halikufanyika

Aliendelea kufafanua kuwa kiapo cha RCO wa Kinondoni SSP David Msangi kilicholetwa Mahakama hapo hakiishawishi Mahakama kuzuia dhamana hiyo, na ikizingatiwa kuwa haki inayobishaniwa Mahakamani hapo ni ya Kikatiba, hivyo Mahakama itaruhusu dhamana itakayoambatana na masharti

Baada ya Mahakama kueleza hayo, upande wa  Jamhuri/ serikali kupitia kwa Wakili wa serikali mwandamizi Job Mrema uliiomba Mahakama kuwa miongoni mwa masharti yanayopaswa kutolewa iwe ni pamoja na mtuhumiwa kunyang’anywa passport ya kusafiria, lakini pia kuiomba Mahakama itoe masharti ya kumtaka mtuhumiwa kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam, kwani endapo mtuhumiwa akiwa huru zaidi yaani kupatiwa dhamana isiyokuwa na masharti ataendelea kutenda makosa zaidi ikizingatiwa kuwa katika Mahakama hiyo kuna shauri lingine linaloendelea ambalo makosa yake yanashabihiana na yale yaliyoko mezani

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Peter Kibatala uliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa si mtu wa kumtilia shaka hata kidogo ikizingatiwa kuwa amewahi kuwa Meya kwenye Halmashauri mbili (2) za Kinondoni na Ubungo, lakini pia akiwa gerezani hivi karibuni amepatiwa nafasi nyingine ya uongozi (Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani), jambo ambalo linadhihirisha kuwa mtuhumiwa huyo anaaminika kwenye jamii

Akijibu hoja ya kukamatwa kwa passport ya kusafiria ya mteja wake Wakili Kibatala ameieleza Mahakama kuwa suala hilo halipaswi kuwa sehemu ya masharti ya dhamana ikizingatiwa kuwa hakuna mwenye uhakika kama mtuhumiwa anamiliki passport ya kusafiria, hivyo Mahakama isije kutoa masharti ambayo baadaye yatakuwa hayatekelezeki yaani yanaelea

Baada ya majibu hayo ya upande wa utetezi, upande wa Jamhuri/ serikali ukiongozwa na Wakili wa serikali mwandamizi Job Mrema uliendelea kuweka msisitizo kwenye hoja zake za awali na kuendelea kuiomba Mahakama kukubaliana na hoja zao, ambapo alitumia fursa hiyo kujenga hoja kuwa majibu ya Wakili wa utetezi yanadhihirisha wazi kuwa hana taarifa na hajawasiliana na mteja wake kuhusiana na hilo ndio maana hajuwi kama anamiliki passport ya kusafiria au hamiliki

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili (2), Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam alitaja masharti matatu (3) ya dhamana kwa mtuhumiwa ambayo yalitekelezwa papo hapo na mtuhumiwa kuachiwa kurejea uraiani

Masharti hayo ni pamoja  na uwepo wa Wadhamini wawili (2) ambao kila mmoja ataweka bond ya shilingi milioni saba za Kitanzania (Tsh. 7,000,000/-), Barua ya Mwenyekiti wa serikali ya mtaa/ Barua ya mwajiri endapo mdhamini atakuwa ni mtumishi wa umma, lakini pia endapo mtuhumiwa anakusudia kusafiri nje ya nchi atalazimika kuitaarifu Mahakama kabla ya kuanza Safari,

Shauri hilo limehairishwa hadi Oktoba 27.2024 ambapo kesi ya msingi inayomkabili Boniface Jacob (Boni Yai) yenye mashtaka mawili (2) inayohusu kuchapisha habari za uwongo kwenye mitandao ya kijamii itaendelea.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!