Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry William Silaa, amewataka Watanzania kutoingiwa na hofu kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoonesha kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepata hasara ya karibu Shilingi bilioni 28.
Akizungumza kupitia kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Jumatano, Aprili 2, 2025, Silaa ameeleza kuwa hasara hiyo si kwa maana ya biashara kushindwa kujiendesha, bali inahusiana na kanuni za kihasibu zinazotumika kwenye mashirika ya umma.
“Kwa Mtanzania wa kawaida, unapozungumzia faida na hasara, unazingatia tu hesabu rahisi za biashara ndogo ndogo. Mfano, ukinunua kuku wa Shilingi elfu 10 kutoka Singida, lazima uangalie nauli yako, gharama ya chakula huko na bei ya kuuza ili upate faida. Lakini kwa mashirika makubwa kama TTCL, hesabu ni tofauti,” amesema Silaa.
Silaa amefafanua kuwa moja ya sababu zilizopelekea TTCL kuonesha hasara ni uhamishaji wa Mkongo wa Taifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda TTCL mnamo Novemba 2023.
“Mkongo huu una thamani kubwa. Unapouhamisha kutoka kwenye vitabu vya wizara kwenda kwenye vitabu vya shirika, moja kwa moja unakuwa umeongeza mali kwenye mizania ya shirika. Sasa, moja ya gharama kubwa zinazotokea ni depreciation (uchakavu),” ameeleza.
Amesema gharama ya uchakavu wa mkongo kwa mwaka mmoja wa fedha ni Shilingi bilioni 36, lakini kwa kipindi cha Novemba 2023 hadi Juni 2024, ilifikia Shilingi bilioni 27.
“Hii bilioni 27 inahesabiwa kama matumizi (expenses) kwenye hesabu za TTCL. Kumbuka pia TTCL tayari ilikuwa na hasara iliyokuwa imebaki (carried forward) ya Shilingi bilioni 4 kutoka mwaka uliopita. Ukijumlisha hizi mbili, unapata ile hasara ya karibu Shilingi bilioni 28 iliyotajwa na CAG,” ameeleza.
Silaa amesema ikiwa hesabu za TTCL zingefanywa kwa njia rahisi ya A-B=C kama biashara ya kuuza kuku, shirika hilo lingekuwa lina faida.
Licha ya ripoti ya CAG kuonesha hasara, Waziri Silaa amesisitiza kuwa TTCL bado linaendelea kujiendesha bila matatizo na linaendelea kutoa huduma kwa Watanzania.
“Kama TTCL ingekuwa inapata hasara kwa maana ya kushindwa kujiendesha, shirika lingesimama au kufungwa. Lakini bado watu wanatumia huduma zake kila siku, mitambo inafanya kazi, mishahara inalipwa, na huduma za mawasiliano zinaendelea,” amesema.
Amesisitiza kuwa ripoti ya CAG itajadiliwa bungeni kupitia kamati za kudumu za Bunge ili kutoa uelewa sahihi kwa Watanzania na kusaidia wabunge kuhoji kwa niaba ya wananchi.
“Ni muhimu kuelewa kwamba hesabu za mashirika makubwa zinafuata viwango vya kimataifa vya kihasibu. Hii ndiyo sababu tunawataka Watanzania wasiingie hofu kuhusu mustakabali wa TTCL,” amehitimisha Silaa