Hali ya sintofahamu imeendelea kutanda mkoani Kigoma kufuatia kifo cha Diwani wa Kata ya Nyamgali kupitia chama cha ACT Wazalendo, Majaliwa Abbas Hamisi, huku kukiwa na mivutano ya kikauli kati ya uongozi wa chama chake na Jeshi la Polisi kuhusu chanzo cha kifo hicho.
Chama cha ACT kimelitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kufanya uchunguzi wa haraka na huru kufuatia kifo hicho. Katika taarifa iliyotolewa Januari 26, 2026, na Katibu wa ACT Kigoma, Yunusa Rashidi Ruhomvya, chama hicho kimeeleza kuwa hakiamini madai kuwa diwani huyo amefariki kwa ajali ya barabarani, bali kimetaja mazingira yanayoashiria mauaji yaliyoratibiwa.
ACT imeeleza kuwa Majaliwa Hamisi alikutwa amefariki tarehe 24 Januari 2026. Hata hivyo, ukaguzi wa mwili uliofanywa na ndugu wa marehemu umeibua maswali mazito. Kwa mujibu wa taarifa ya chama, mwili wa marehemu haukuwa na michubuko wala majeraha yanayotokana na ajali, koti alilovaa lilikutwa pembeni ya mwili wake barabarani, laini za simu yake zilitolewa na hazikuonekana, huku simu ikikutwa peke yake na kwamba shingoni mwa marehemu kulionekana alama zinazoashiria kunyongwa.
ACT Wazalendo imelaani vikali mfululizo wa matukio ya mauaji, ikiamini kuwa yanatokana na ushindani wa kisiasa. Katibu Ruhomvya amesisitiza kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhisho la kuzima madai ya haki na demokrasia nchini.
“Ndugu wa marehemu pamoja na chama chetu tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kufanya uchunguzi huru wa mauaji haya ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwani familia na Chama hatuamini kuwa kifo chake kimetokana na ajali bali kulikuwa na njama zilizoratibiwa makhsusi ya kufanyika kwa mauaji ya Diwani wetu”, amesema Ruhomvya katika tamko hilo.
Chama hicho kimefananisha tukio hili na matukio mengine ya awali kama lile la Asante Nyerere, kikitaka vyombo vya usalama kuhakikisha haki inatendeka haraka ili kurejesha imani kwa wananchi na familia ya marehemu ambaye amezikwa jana tarehe 25 Januari 2026.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limepinga vikali madai hayo likiyataja kama upotoshaji unaolenga kuzua taharuki, likisisitiza kuwa kifo hicho kimesababishwa na ajali ya barabarani na si vinginevyo.
Katika taarifa iliyotolewa Januari 27, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP Philemon Makungu, jeshi hilo limeeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 23 Januari, 2026, majira ya saa nne usiku katika Kijiji cha Songambele. Marehemu alikuwa akiendesha pikipiki namba MC 709 BCW aina ya Kinglion kabla ya kugongwa na gari ambalo bado halijafahamika.
Polisi wamebainisha kuwa askari waliofika eneo la tukio walikuta mwili wa marehemu ukiwa barabarani sambamba na pikipiki yake iliyoharibika vibaya. Aidha, mahindi aliyokuwa amebeba marehemu yalikutwa yamemwagika na kusambaa eneo lote la ajali, jambo linalothibitisha kutokea kwa mgongano huo.
Kufuatia madai ya chama cha ACT Wazalendo kuwa kifo hicho kina utata na kina alama za kunyongwa, Jeshi la Polisi limewataka watu wanaoeneza taarifa hizo kuacha upotoshaji unaolenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi na ndugu.
“Kutokana na tuhuma zilizosambazwa…Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa na ushahidi wa kweli tofauti na ambao umekusanywa hadi sasa kutoka eneo la tukio na kutoka kwa waliotoa taarifa baada ya kukuta ajali hiyo, aufikishe Polisi ili uweze kufanyiwa kazi kwa haraka”, imeeleza taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji wa kina ili kubaini gari iliyomgonga marehemu pamoja na dereva aliyekuwa anaiendesha ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa. Polisi wamehitimisha kwa kuonya kuwa hawatasita kuchukua hatua dhidi ya wale wanaotumia matukio ya huzuni kama hayo kuzua hasira miongoni mwa wananchi bila kuwa na uhakika au ushahidi wa wanachokisambaza.
“Kama kweli wana ushahidi wa kweli kuhusiana na taarifa za kifo kama hiki azifikishe kwenye mamlaka husika na siyo kujenga chuki zinazoweza kusababisha hasira na taharuki wakati hana uhakika au ushahidi wa anachoeleza na anacho sambaza kupitia mitandao ya kijamii”, wameeleza Polisi.